Nchi za magharibi kuzungumza na Iran
26 Septemba 2013Mkutano huo utakaofanywa pembezoni mwa mkutano wa baraza kuu la umoja wa Mataifa mjini New York, unanuia kutoa fursa kwa duru ya kwanza ya mazungumzo yenye tija pengine mwezi ujao tangu ya mwisho yaliyofanyika mwezi Aprili.
Mkutano wa leo pia utakuwa wa kwanza wa ngazi ya juu wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, kukutana ana kwa ana na mwenzake wa Iran, Javad Zarif, kwani nchi hizo mbili hazijaweza kukaa chini pamoja kwa miaka mingi sasa kufuatia uhasama wa kidiplomasia.
Mkutano kipimo cha azma ya Iran
Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi, China na Ujerumani zitashiriki katika mkutano ulioandaliwa na mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya, Bi Catherine Ashton. Urusi na China pia zinatarajiwa katika mkutano huo.
Haya yanawadia kufuatia kufufuliwa kwa matumaini ya kupatikana ufumbuzi wa mzozo huo wa mpango wa kinyuklia baada ya rais mpya wa Iran, Hassan Rouhani, aliye na msimamo wa wastani, kuashiria kuwa nchi yake iko tayari kwa mazungumzo na nchi za magharibi.
Rais wa Marekani, Barrack Obama, amemuagiza Kerry kushughulikia uwezekano wa kufufuliwa kwa mazungumzo yatakayotatua mzozo huo wa kinyuklia na kusisitiza kuwa Iran sharti ithibitishe kuwa kweli ina nia ya kupatikana kwa suluhisho.
Rouhani mapema wiki hii katika hotuba yake ya kwanza katika baraza la umoja wa Mataifa alisema nchi yake haina cha kuficha kuhusiana na mpango wake wa kinyuklia kwani lengo lao sio kuwa kitisho kwa ulimwengu.
Palipo na nia pana njia
Kiongozi huyo wa Iran amesema iwapo kuna nia ya kisiasa kutoka nchi za magharibi basi nchi yake iko tayari kwa mazungumo na anaamini kuwa mzozo huo unaweza kutatulika kupitia mazungumzo hayo.
Rouhani ameongeza kuwa anatarajia makubaliano kuafikiwa katika kipindi cha miezi mitatu au sita ijayo na kusisitiza kuwa azma yake hiyo inaungwa mkono na kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ali Khamenei.
Ashton amesema amefurahishwa na azma na juhudi za waziri wa mambo ya nje wa Iran lakini akaongeza mengi bado yanahitajika kufanywa.
Nchi hizo za magharibi zilitoa pendekezojipya kwa Iran mapema mwaka huu kabla ya kuchaguliwa kwa Rouhani linaloaminika kuwa lina lengo la kulegeza vikwazo vilivowekewa nchi hiyo na kuathiri uchumi wake na badala yake Iran ipunguze uzalishaji wake wa madini ya Uranium.
Mwandishi:Caro Robi/afp/ap
Mhariri: Josephat Charo