Nchi za magharibi hazina la kufanya wakati Libya ikiteketea
4 Agosti 2014Makabiliano makali baina ya makundi hasimu ya wapiganaji yakitishia kuipasua nchi hiyo katika vipande na kuitumbukiza katika hali ya kutokuwa na amani. Baada ya kifo cha Gadafi mnamo Oktoba 2011 kufuatia vita baina ya wanajeshi wake na waasi walioungwa mkono na Wamarekani, Waingreza, Wafaransa na nchi kadhaa za Kiarabu, mataifa ya magharibi yaliandaa mikutano kadhaa ya kuijenga upya Libya na kuliimarisha jeshi lake. Lakini pendekezo la nchi za magharibi kutaka kuisaidia Libya liligonga ukuta, huku Walibya ambao walipata uhuru wao kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Italia mwaka wa 1951, wakidhamiria kuhifadhi uhuru wao na kuondoa uingiliaji wa kigeni.
Na watalaamu wanasema ni kutokana na kushindwa kulifanyia marekebisho jeshi na kuimarisha uchumi wake baada ya kuangushwa Gaddafi ambako kumeruhusu migogoro kuchipuka tena nchini humo. Mapigano mapya baina ya makundi hasimu yanayogombania udhibiti wa taasisi muhimu za serikali yamesababisha vifo vya watu wengi katika kipindi cha wiki tatu zilizopita na kuzilazimu nchi kadhaa za magharibi kuwahamisha raia wake kutoka katika nchi hiyo iliyoparaganyika.
Jason Pack ni mtafiti kuhusu Libya katika Chuo Kikuu cha Cambridge na anasema nchi za magharibi zilikuwa na nia ya kutoa msaada zaidi, lakini kama tu Walibya wenyewe wangeuitisha. Kwa hivyo hawakupata msaada huo kwa sababu hawawezi kulazimishiwa. Pack anaongeza kuwa mapigano ya kindani yanayotakana na serikali kuu kuwatuliza wapiganaji na kuonekana kuyatekeleza masharti yao, kiasi kwamba wapiganaji hao wana mamlaka yote na serikali kuu kimsingi haipo tena.
Naye Antoine Vitkine ambaye ameandika vitabu kdhaa na kutengeneza filamu kuhusu Libya, anasema Walibya walikuwa wakisema na bado wanasema “hii ni nchi yetu”. walikuwa na hamu ya kuijenga wenyewe”. Mchambuzi huyo anaongeza kusema kuwa jibu la viongozi walioingia madarakani baada ya kuangushwa Gaddafi lilikuwa ni: “ni wajibu wetu na kwetu sisi kutengeneza mambo”.
Wachambuzi pia wanasema kuwa tofauti za kitamaduni na kitaasisi zilizokita mizizi pia zinaongeza katika tatizo hilo. Jean-Yves Moisseron kutoka taasisi ya Ufaransa ya Utafiti na Maendeleo anasema “dhana ya utaifa haina maana nchini Libya”. Ukabila na malumbano ya ndani ya kugombania mali ya raslimali ya mafuta nchini humo – ambayo ni kubwa zaidi barani Afrika – vimechangia kwa kiasi kikubwa katika mchafuko ya sasa nchini Libya. Moisseron anasema makundi ya kikabila hayakubali ugawanaji wa raslimali katika mfumo wake wa sasa. Na sasa mgogoro wa Libya umefikia kilele kati ya wale wanaodhibiti raslimali za nchi na wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu.
Mjumbe wa zamani wa Ufaransa Patrick Haimzadeh, ambaye alifanya kazi mjini Tripoli, anasema nchi hiyo imefikia kiwango cha kusambaratika. Anasema hakuna anayefahamu kitakachotokea katika miaka kumi ijayo nchini Syria, Libya na Iraq, makolonyo yote ya zamani ambayo yaliumia au yanaumia kutokana na tawala za kimabavu au kama yataendelea kuwepo.
Wakati mgogoro na machafuko yakiendelea nchini Libya, swali linalojitokeza hapa ni kama hatua ya nchi za Magharibi kuingilia kati kijeshi ilikuwa ni kosa. Haimzadeh anasema Wamarekani waligundua kuwa baada ya Afghanistan na Iraq, uingiliaji kati kijeshi hautatui lolote. Jee, kuna mtu angewaacha maelfu ya watu waliokuwa wamezingirwa na majeshi ya Gaddafi mjini Beghazi wauawe kinyama? Anauliza Vitkine akimaanisha hali iliyochochea operesheni ya jeshi la kimataifa ya Machi 2011. Stefano Silvetri kutoka taasisi ya masuala ya Italia anasema ilikuwa hatua mwafaka, lakini kushindwa kuituliza hali baada ya operesheni hiyo bila shaka ilikuwa kosa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo