1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za kiislamu kupunguza migawanyiko ya kimadhehebu

Caro Robi15 Aprili 2016

Rais wa Uturuki Tayyip Recep Erdogan anahitimisha mkutano wa viongozi wa nchi za kiislamu unaolenga kupunguza tofauti za kimadhehebu hasa kuhusu mizozo ya Syria na Yemen na kushughulikia kitisho cha ugaidi.

https://p.dw.com/p/1IWMF
Picha: Getty Images/AFP/O. Kose

Katika dhifa ya chakula cha jioni hapo jana aliyowaandalia viongozi wa nchi za kiislamu wanaohudhuria mkutano huo wa kilele wa jumuiya ya ushirikiano ya mataifa ya Kiislamu OIC, Rais Erdogan amekariri haja ya kuwepo umoja na mshikamano miongoni mwa waislamu wote.

Erdogan amesema lengo ni kuwapa waislamu matumaini kuhusu siku za usoni na kutokana na mkutano huo, wanatarajia ukurasa mpya utafunguliwa.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano huo wa OIC ni Mfalme Salman wa Saudi Arabia na Rais wa Iran Hassan Rouhani ambao nchi zao zimekuwa zikitofautiana vikali na kuchukua misimamo tofauti kuihusu mizozo ya Yemen na Syria.

Wasunni na Washia wahimizwa kupendana

Rais Rouhani ambaye pia alizungumza katika mkutano huo amesema hakuna ujumbe ambao unachochea mgawanyiko miongoni mwa Waislamu unapaswa kutolewa katika mkutano huo.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Getty Images/AFP/K. Ozer

Uturuki inayoutazama mkutano huo kama jukwaa la kuinua hadhi yake katika ulimwengu wa kiislamu pia nchi hiyo imepata fursa ya kuwaleta pamoja waislamu takriban bilioni 1.7 kutoka duniani.

Erdogan ambaye nchi yake inashikilia wadhifa wa uenyekiti wa OIC kwa kipindi cha miaka miwili ijayo anatarajiwa kuongoza kikao cha mwisho cha mkutano huo ulioanza tangu jana leo kabla ya kufanya mkutano na wanahabari.

Viongozi hao wa nchi takriban 30 za kiislamu wamekubaliana kushirikiana zaidi katika kupambana dhidi ya ugaidi na uhalifu mwingine na kuundwa kwa kituo cha kushughulikia ushirikiano zaidi wa polisi wa nchi wanachama wa OIC ambacho kitaanzishwa Istanbul.

OIC ina nchi wanachama 57

Mkutano huo wa OIC unakuja wakati ambapo Uturuki inaonekana kutafuta ushirikiano zaidi na Saudi Arabia. Hapo jana mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili walitia saini makubaliano ya maelewano kuhusu kuundwa kwa baraza la ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya OIC
Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya OICPicha: Reuters/M. Sezer

Uturuki, Saudi Arabia na Qatar zinawaunga mkono waasi wanaompinga Rais wa Syria Bashar al Assad. Kwa upande mwingine Iran na Urusi ambayo ina uhusiano mbaya katika siku za hivi karibuni na Uturuki zinauunga mkono utawala wa Rais Assad.

Wachambuzi wameonya kuwa Uturuki inapaswa kutahadhari kuhusu ushirikiano wake na Saudi Arabia ili isije ikaonekana kuwa na uhusiano wa misingi ya kimadhehebu unaoilenga Iran.

Katika hatua ya Uturuki kujaribu kusawazisha hali, Rais Rouhani anatarajiwa kuanza ziara rasmi Uturuki ya kuimarisha uhusiano kati ya Iran na Uturuki punde baada ya kukamilika kwa mkutano huo wa kilele wa OIC. Shirika hilo la ushirikiano wa mataifa ya kiislamu lina wanachama 57.

Mwandishi: Caro Robi/afp

Mhariri: Yusuf Saumu