1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi zenye mazingira magumu kwa waandishi wa habari

Sylvia Mwehozi
3 Mei 2018

Ikiwa leo ni siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, barani Afrika hali ni ya mchanganyiko, baadhi ya nchi zimepiga hatua na nyingine zikishamiri katika ukiukaji wa uhuru wa vyombo vya habari.

https://p.dw.com/p/2x5QP
Kenia Symbolbild keine Pressefreiheit in Afrika
Picha: picture alliance/AP Photo/S. Azim

Ghana ni nchi ya juu Afrika katika faharasi ya dunia ya uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka 2018, iliyoandaliwa na shirika la Maripota wasio na mipaka, wakati Eritrea ikiwa nafasi ya mwisho katika viwango vya dunia.

Nchini Eritrea uhuru wa vyombo vya habari unachukuliwa kuwa haupo, baada ya kuanguka mwaka 2001 wakati serikali ilipofanya ukandamizaji wa kikatili dhid ya vyombo vya habari binafsi, kulishuhudiwa wimbi la kamata kamata. Rais Isias Afeworki anajulikana zaidi kama "mwindaji" wa uhuru wa vyombo vya habari na kutumia vyombo vya habari vya kitaifa kama mdomo wake. Waandishi, watangazaji na wasanii wanafuatiliwa na taarifa zinazuiwa kufika kwa wananchi.

Ukanda wa Afrika Magharibi

Serikali ya Cameeron imetaja mitandao ya kijamii kama "aina mpya ya ugaidi" na kuifunga mara kwa mara. Watangazaji wa Radio na Televisheni walifungiwa kwa wiki mbili mwezi Machi katika uchaguzi wa marudio. Magazeti yanayochapisha ripoti zinazowakera maafisa wa serikali yanafungiwa na waandishi, wachapishaji wanakamatwa.

Sambia Zeitung The Post - Joan Chirwa-Ngoma & Mukosha Funga
Waandishi wa habari Zambia wakipelekwa kizuiziniPicha: Getty Images/AFP/D. Salim

Sudan inazingatia kile kinachoitwa udhibiti kabla ya uchapishaji, kuwaweka kizuizini waandishi na kuingilia kwa uwazi uzalishaji wa habari. Sheria ya uhuru wa taarifa ya mwaka 2015 imekataliwa kama njia nyingine ya udhibiti wa serikali wa taarifa za umma. Waandishi wa habari wanapaswa kufaulu mtihani na kuomba kibali cha kufanya kazi.

Nchini Chad waandishi wa habari hukamatwa kiholela, kushambuliwa na kutishiwa. Katika miezi ya karibuni serikali ilifungia majukwaa ya mitandao ya kijamii na wanaharakati wa mitandaoni. Mtandao wa Intaneti ulizimwa nchini kote tangu Machi 28. Ilifuatiwa kuzimwa kwa intaneti kabla ya maandamano ya asasi za kiraia na maandamano ya vyombo vya habari yaliyopewa jina la "siku bila ya vyombo vya habari".

Niger, waandishi huru wa ndani na wale wa kigeni wanakabiliwa na ugumu wakati wanapojaribu kutekeleza kazi zao. Vikosi vya usalama huharibu vifaa na kuvuruga kazi zao. Vile vinavyomilikiwa na watu binafsi havina haki ya kupata matangazo.

Hali katika nchi za Afrika Mashariki

Sudan Kusini waandishi wa habari wanalazimishwa na serikali kuepuka kuandika habari zinazohusu mgogoro. Vyombo vy ahabari vya nje vimeripotiwa kunyanyaswa na kupigwa marufuku kutoka taifa hilo changa, ambako karibu waandishi wa habari 10 wameuawa tangu mwaka 2011.

Huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, mashirika yanayofuatilia vyombo vya habari yanasema waandishi wameuwawa, kupigwa, kukamatwa na kutishiwa tangu rais Jospeh Kabila alipochukua madaraka kutoka kwa baba yake mwaka 2001. Vyombo vya habari vya kimataifa vimelalamika kwamba serikali mara nyingi inaingilia au kuzima matangazo. Maandamano ya upinzani yalisababisha serikali kuzima intaneti.

Azory Gwanda - Journalist (Mwananchi Communications Limited (MCL) in Tanzania
Mwandishi wa habari wa Tanzania Azory Gwanda aliyepotea katika mazingira ya kutatanishaPicha: Privat

Taifa la Burundi, ukandamizaji wa serikali kuelekea uhuru wa vyombo vya habari na waandishi ni mkubwa sana. Vyombo vya habari vya umma vinazidi kuchukua nafasi ya vile vya binafsi kwasababu vililazimishwa kufunga wakati wa jaribio la mapinduzi miaka mitatu iiyopita. Mamia ya waandishi wameikimbia nchi tangu mwaka 2015, wengi wako Rwanda, Kenya na Ubelgiji.

Nchini Tanzania wakosoaji wanasema rais John Magufuli amelenga moja kwa moja kuzuwia uhuru wa kujieleza tangu aingie madarakani mwaka 2015. Waandishi wamekamatwa au kupotea moja kwa moja. Makampuni ya habari yamefungiwa kwa kipindi cha muda mrefu na magazeti kuzuiwa kuchapisha habari. Sheria dhidi ya vyombo vya habari zimezidi kuwa kali.

Swaziland, taifa hilo la kifalme linajulikana kwa kuzuia upatikanaji wa taarifa na kuwazuia waaandishi kutekeleza wajibu wao kikamilifu. Kuna sheria kali dhidi ya vyombo vya habari na waandishi mara nyigi wanajikuta mahakamani kutokana na ripoti zao. Mhariri mmoja hivi karibuni ameikimbia nchi baada ya kuripoti juu ya mikataba ya biashara haramu inayohusishwa na mfalme Mswati III.

Serikali ya Ethiopia ina vikwazo dhidi ya vyombo vya habari na waandishi wanafanya kazi katika mazingira magumu. Sambamba na Eritrea, nchi hii ina kiwango kikubwa cha waandishi  waliokamatwa katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara. Majukwaa ya mitandao ya kijamii wakati mwingine hufungiwa na serikali na vyombo vya habari vya nje mara nyingi vimekuwa vikilengwa.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dw

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman