Nchi nyingi zatarajia kuviondoa vikwazo vya COVID 19
3 Februari 2022Sweden imetangaza kuwa itaviondoa vikwazo hivyo wiki ijayo licha ya kushuhudia rekodi ya maambukizi. Nchi hiyo inaamini kuwa dozi ya tatu ya chanjo na idadi ya maambukizi ya COVID-19 ya hapo awali, vitasaidia kudhibiti idadi ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini.
Vizuizi vya sasa, ambavyo ni pamoja na kufungwa mapema kwa migahawa na kutozidisha idadi ya watu 500 ndani ya makumbi makubwa, viliongezwa muda mwezi uliopita hadi Februari 9. Waziri Mkuu wa Sweden Magdalena Andersson amewaambia waandishi wa habari kuwa sasa ni wakati wa kuifungua Sweden tena na kusisitiza kuwa matokeo mabaya ya maambukizi wameyavuka.
soma zaidi: Maambukizi ya Covid yapindukia laki 2 kwa siku Ujerumani
Nae Waziri Mkuu wa jamhuri ya Czech amesema kuanzia wiki ijayo, nchi hiyo itasitisha hatua ya ulazimu wa kuonyesha vyeti vya chanjo ili kuingia kwenye migahawa na kumbi za starehe na hatua hiyo itawahusu pia hata watu ambao hawajachanjwa.
Nchi hiyo yenye watu takriban milioni 10, ambayo hapo awali iliathirika mno na janga la COVID, inashuhudia tena ongezeko la idadi yamaambukizi wakati ambapo aina mpya ya kirusi cha Omicron ikitapakaa. Hata hivyo, maafisa wanatarajia kuwa mwezi huu maambukizo yatapungua.
Serikali ya New Zealand yalegeza masharti ya kupambana na COVID 19
Serikali ya New Zealand imesema siku ya Alhamisi kuwa itaondoa sheria za karantini kwa wasafiri wanaoingia nchini humo na kufungua tena mipaka yake, hatua iliyopokelewa kwa shangwe na maelfu ya raia wa nchi hiyo waliopo nje ya nchi na ambao wamevumilia muda mrefu wakisubiri kurejea nchini mwao.
Tangu kuanza kwa janga hili, New Zealand imekuwa miongoni mwa nchi duniani yenye sheria kali za udhibiti wa mipaka. Wasafiri wanaoingia nchini humo wanahitaji kukaa karantini kwa siku 10 katika chumba cha hoteli inayolindwa na wanajeshi.
soma zaidi: Aina mpya ya kirusi cha Omicron yaripotiwa
Hata hivyo janga la virusi vya corona bado linaiandama dunia. Mfano nchini Urusi, kumeripotiwa siku ya Alhamisi visa zaidi ya laki moja na nusu vya maambukizi kwa siku moja na idadi ya vifo 667 ndani ya saa 24 zilizopita.
Wakati huohuo, jopo la wataalamu wa Ujerumani kuhusu matumizi ya chanjo (STIKO), linajiandaa kupendekeza dozi ya nne ya chanjo ya COVID-19. Mkuu wa kamati hiyo, Thomas Mertens, amewaambia wanahabari kuwa wanazo data kutoka Israeli zinayoonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa, dozi ya nne inaboresha ulinzi kwa aina kali ya virusi na kuwa wanatarajia kuwasilisha
mapendekezo hayo hivi karibuni.
Vyanzo: rtre,ape