Nchi kadhaa zachukua tahadhari ya janga la virusi vya Corona
27 Februari 2020Australia imeanzisha hatua za dharura na taiwan imepandisha kiwango cha kuchukua hatua kuhusu janga hilo kwa kiwango cha juu, siku moja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kumteua makamu wake wa rais Mike Pence, katika nafasi ambayo atahusika na mapambano dhidi ya mzozo huo wa kiafya unaoikabili dunia.
Marekani na Korea kusini zimeahirisha luteka yao ya pamoja ya kijeshi ili kupunguza kusambaa kwa virusi hivyo, ambavyo vimejitokeza katika maeneo ya mbali na China, sehemu virusi hivyo vilipoanzia , katika soko linalouza nyama za wanyama pori katika mji wa Wuhan.
Waziri mkuu wa Australia Scott Morrison amesema nchi yake , ambayo ina watu 23 walioambukizwa virusi hivyo, inachukua hali hiyo katika kiwango cha janga na mahospitali yamepewa amri kuhakikisha madawa ya kutosha yanapatikana, pamoja na vifaa vya kuwakinga wauguzi na wafanyakazi.
Masoko ya hisa yameporomoka zaidi, bei ya mafuta pamoja na hati fungani za serikali ya Marekani zikiingia katika hali ya mdororo wakati ishara zaidi za kusambaa kwa virusi hivyo duniani zikiongeza hofu ya kutokea janga la mzozo huo.
Watu zaidi ya 80,000 wameambukizwa virusi vya corona , na watu 2,800 wamefariki, wengi wao nchini China. Korea kusini imeripoti watu 171 walioambukizwa, na kufikisha watu 1,766 kwa jumla walioambukizwa. China imeripoti watu wapya 433 walioambukizwa na watu wengine 29 wamefariki.
Iran haitaiweka miji katika karantini
Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema jana kuwa nchi hiyo haina mipango ya kuweka miji yake katika karantini kutokana na maambukizi na vifo nchini humo kutokana na virusi vya corona, ambapo wizara ya afya imesema watu 19 wamefariki nchini humo.
Saudi Arabia imesitisha leo utoaji wa visa kwa watu wanaofanya ziara katika maeneo matakatifu kwa ajili ya ibada ya hija ndogo ya Umrah, hatua ambayo imesababishwa na hofu ya virusi vya Corona na pia kuna wasi wasi kuhusu ibada ya kila mwaka ya hija.
Nchi hiyo ya kifalme , ambayo inakuwa mwenyeji wa mamilioni ya mahujaji kila mwaka katika miji ya Mecca na Medina , pia imesitisha visa kwa watalii kutoka katika nchi ambazo zimeripotiwa kuwa na maambukizi wakati hofu ya kutokea janga la virusi hivyo ikiongezeka.
Shirika la taifa la utalii nchini Urusi leo limelitaka shirika la taifa la safari za kitalii kusitisha safari hizo zote kwenda Italia, Korea kusini na Iran hadi pale suala hilo la virusi vya corona litakapodhibitiwa katika nchi hizo.