Yanayojiri kuhusu virusi vipya vya corona
26 Novemba 2021Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema siku ya Ijumaa kwamba Tume hiyo itapendekeza kwa nchi wanachama, kuchukua hatua kwa pamoja kusitisha usafiri wa anga kutoka na kwenda eneo la kusini mwa Afrika kutokana na kuripuka kwa aina hiyo mpya ya virusi vya corona. Tume ya Utendaji inatarajia kuwa nchi zote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zitapitisha azimio hilo haraka ili liweze kuidhinishwa na Baraza la Ulaya.
Wakati huo huo Uingereza tayari imepiga marufuku kwa muda safari za ndege kutoka kwenye nchi kadhaa barani Afrika. Nchi hizo ni Afrika Kusini, Namibia, Botswana, Zimbabwe, Lesotho na Eswatini. Kuanzia Ijumaa imewataka wasafiri wa Uingereza wanaorejea kutoka kwenye maeneo hayo kukaa karantini. Afrika Kusini imelalamikia marufuku hiyo ya Uingereza imesema imechukuliwa haraka mno.
Kwingineko washauri wa Shirika la Afya Duniani WHO wanafanya kikao maalum ili kuwasilisha taarifa kuhusu hali ya wasiwasi kutokana na virusi vipya vya corona. Msemaji wa shirika la afya duniani Christian Lindmeier amesema katika swala la kuweka vizuizi vya usafiri, ni muhimu kutambua kwamba nchi zinaweza kufanya kazi pamoja na nchi zilizoathiriwa na kushirikiana kimataifa kufanya kazi za kisayansi, ili kupambana na janga hili na kulielewa zaidi. Msemaji WHO amesema shirika hilo litatoa mwongozo zaidi kwa serikali juu ya hatua zinazoweza kuchukuliwa.
Huko nchini Israel wizara ya afya imesema mtu aliyeambukizwa virusi hivyo vipya vya corona amethibitishwa nchini humo. Mtu huyo aliwasili nchini humo kutoka Malawi. Wizara ya afya ya Israel imesema watu wengine wawili wanaodhaniwa kuwa wameambukizwa na virusi hivyo wamewekwa karantini wakisubiri matokeo ya vipimo.
Wakati huo huo masoko ya hisa barani Ulaya leo yamo hatarini kukabiliwa na kipindi cha mashaka makubwa kabisa ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja baada ya kupatikana taarifa juu ya maambukizi ya virusi vipya yya corona. Inahofiwa, virusi hivyo vinavyoweza kuwa sugu dhidi ya chanjo vimesababisha wasiwasi na kuathiri uchumi wa dunia. Taarifa juu ya virusi hivyo vimewafanya wawekezaji waondoe vitega uchumi kutoka kwenye mali zenye mashaka.
Vyanzo: /RTRE/DPA/AP