Nchi ambazo wanawake wanaongoza
Katika mataifa huru 195 duniani, mengi bado yanaongozwa na wanaume katika nafasi mbalimbali kama vile Rais, Kansela, na waziri mkuu. Wanawake bado ni wachache katika nafasi za uongozi.
Kansela Angela Merkel
Merkel mwenye umri wa miaka 62 alichaguliwa kuwa Kansela wa Ujerumani mwaka 2005, ni kiongozi wa kwanza mwanamke kuongoza shirikisho la Ujerumani. Jarida la Time limemtaja Merkel ambaye pia ni mtoto wa mchungaji kutoka iliyokuwa Ujerumani Mashariki kuwa ni mmoja kati ya wanawake wenye uwezo zaidi duniani. Pia alichaguliwa kuwa "mtu wa mwaka 2015"
Theresa May
Theresa May ni waziri mkuu wa pili mwanamke wa Uingereza baada ya Margaret Thatcher aliyeongoza miaka ya 1980. May mwenye umri wa miaka 60 amewahi pia kuwa waziri wa mambo ya ndani. Alichukua wadhifa huo mpya mwezi Julai mwaka 2016 wiki chache baada ya Uingereza kupiga kura ya kujitoa Umoja wa Ulaya. May anakabiliwa na jukumu zito la kuhakikisha nchi yake inatoka vyema katika muungano huo.
Tsai Ing-wen
Tsai Ing-Wen ni Rais wa kwanza mwanamke kuongoza kisiwa kidogo cha Taiwan, baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais mwezi Mei, 2016. Kuchaguliwa kwa Tsai ambaye ni mkosoaji wa China, kuliifanya China kusitisha uhusiano wake na Taiwan-mshirika mkubwa wa Marekani. Tsai Ing-Wen ameweka wazi kuwa hatakubali shinikizo kuhusu uhuru wa Taiwan.
Ellen Johnson Sirleaf
Ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa urais barani Afrika, Sirleaf mwanamke mwenye umri wa miaka 78 amekuwa rais wa Liberia tangu mwaka 2006. Mwaka 2011, Sirleaf na wanawake wanaharakati wawili kutoka Liberia and Yemen walitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel kwa juhudi zao zisizo za matumizi ya nguvu, kwa usalama wa wanawake na haki za wanawake katika ushiriki wa kujenga amani.
Dalia Grybauskaite
Dalia Grybauskaite ni mwanamke wa kwanza kuongoza taifa dogo la Lithuania, Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 60 pia ni mcheza karate aliyefika hatua ya mkanda mweusi na amekuwa akitambulika kama "mwanamke wa shoka. Grybauskaite amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali kabla ya mwaka 2009 kuchaguliwa kuwa rais na mwaka 2014 kuchaguliwa tena.
Erna Solberg
Norway pia inaongozwa na mwanamke. Erna Solberg alianza kutumikia wadhifa huo mwaka 2013. Solberg mwenye umri wa miaka 55 ni waziri mkuu mwanamke wa pili kwa utajiri kutoka upande wa kaskazini baada ya Gro Harlem Brundtland. Msimamo wake kuhusu sera ya watu wanaoomba hifadhi umempatia jina la utani la "chuma Erna" kiongozi huyo wa chama cha kihafidhina.
Beata Szydlo
Ni waziri mkuu wa tatu wa Poland ambaye amekuwa katika nafasi hiyo kwa karibu mwaka mmoja sasa. Kipaumbele cha serikali yake ni kuhakikisha usalama wa wapoland na kuchangia usalama wa Umoja wa Ulaya. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 53, katika hotuba yake ya kwanza bungeni alisema ni mwanasiasa mwenye uzoefu na Mkristo wa kanisa Katoliki.
Saara Kuugongelwa-Amadhila
Saara Kuugongelwa-Amadhila mwenye umri wa miaka 49 ni waziri mkuu wa nne wa Namibia, alishika wadhifa huo tangu mwaka 2015. Akiwa kijana alikimbilia uhamishoni Sierra Leone na baadaye kuendelea na masomo yake nchini Marekani. Alihitimu shahada ya kwanza ya sayansi na uchumi kabla ya kurejea nyumbani mwaka 1994. Ni mwanamke wa kwanza kuongoza Serikali nchini Namibia.
Park Geun-hye
Park Geun-hye ni mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa rais wa Korea Kusini, ana umri wa miaka 64 na ameshika wadhifa huo tangu mwaka 2013. Mwaka huo huo jarida la Forbes lilimuongeza katika idadi ya wanawake wenye nguvu zaidi duniani. Baba yake Park Chung-hee, amewahi kuwa rais wa nchi hiyo mwaka 1963 mpaka 1979.
Michelle Bachelet
Michelle Bachelet amekuwa rais wa Chile tangu mwaka 2014, sasa ukiwa ni muhula wake wa pili. Michelle Bachelet ambaye amesomea utabibu, amewahi kutumikia kifungo kilichoambatana na mateso akiwa kijana. Amewahi pia kuishi uhamishoni nchini Australia na Ujerumani Mashariki:
Sheikh Hasina Wajed
Jarida la Forbes limemuongeza pia waziri mkuu wa sasa wa Bangladesh katika idadi ya wanawake 100 wenye nguvu duniani kwa mwaka 2016. Sheikh Hasina Wajed ana mamlaka katika nchi yake ambayo ni nchi ya nane kwa kuwa na idadi ya watu wengi duniani, Bangladesh ina jumla ya watu milion 162. Sheikh Hasina amekuwa katika mamlaka hayo tangu mwaka 2009.
Kolinda Grabar-Kitarovic
Kolinda Grabar-Kitarovic mwenye umri wa miaka 48 amewahi kushika nyadhifa mbalimbali na pia amewahi kufanya kazi kama balozi wa Croatia nchini Marekani kabla ya kuchaguliwa kuwa rais wa kwanza mwanamke wa nchi yake mwaka 2015. Grabar-Kitarovic ni mwanamke wa kwanza pia kuwahi kufanya kazi NATO kama kaimu katibu mkuu wa masuala ya diplomasia kwa umma wadhifa alioshika mwaka 2011 mpaka 2014.