Navalny aapa kurudi Urusi
1 Oktoba 2020Mahojiano hayo alifanyiwa na gazeti la kila wiki la Der Spiegel la Ujerumani na sehemu ya mahojiano hayo iliyochapishwa kwenye tovuti ya gazeti hilo leo alhamisi,Navalny amenukuliwa akisema ana uhakika kwamba Putin yuko nyuma ya kitendo hicho na hana maelezo mengine.
Navalny alisafirishwa mpaka mjini Berlin nchini Ujerumani alikoletwa kutibiwa baada ya kuzirai na kupoteza fahamu mnamo mwezi Agosti wakati akiwa kwenye ndege kutoka Tomsk kwenda Moscow Urusi baada ya ziara yake ya kampeini ya kuwaunga mkono wagombea wa upinzani katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mkosoaji huyo wa serikali ya Urusi aliruhusiwa kutoka hospitali kiasi zaidi ya wiki moja iliyopita na matamshi yake ya kwanza aliyotowa mbele ya waandishi habari yanakuja wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana katika mkutano wa kilele ambapo suala juu ya namna ya kuijibu Urusi hueda likazuka kuhusiana na kisa hiki cha Navalny.
Ufaransa na Sweden zaunga mkono uchunguzi wa Ujerumani
Ujerumani ambayo inashikilia hivi sasa uongozi wa Umoja wa Ulaya imeshasema kwamba majibu ya vipimo vya sumu yanaonesha Navalny alilishwa sumu ya kuharibu msihipa ya fahamu ya Novichok,ambayo ikitumika sana enzi za muungano wa Sovieti.
Kadhalika Ufaransa na Sweden zote kila mmoja kivyake ameunga mkono matokeo ya uchunguzi huo wa Ujerumani. Na kama haitoshi serikali ya Kansela Angela Merkel pia imeshaionya Moscow juu ya uwezekano wa kuwekewa vikwazo ikiwa itashindwa kuchunguza kikamilifu kadhia hiyo.
Na katika ishara ya kuonesha ni kwa jinsi gani analichukuliwa kwa uzito suala hili,Knasela Merkel binafsi aliwahi kumtembelea Navalny katika hospitali ya Charite mjini Berlin alikokuwa akitibiwa.
Urusi imekanusha kabisa kuhusika na kunyweshwa sumu Navalny
Mkosoaji huyo wa Putin tangu alipotoka hospitali anaonekana kushughulika sana mitandaoni ambapo katika ujumbe mmoja alioutuma kwenye blogu alisema mahabara tatu za Ulaya zimekuta sumu ya Novichok mara kadhaa kwenye mwili wake.Lakini akaongeza kusema kwamba Urusi bado haijaanzisha uchunguzi wa aina yoyote lakini pia akasema hategemea kuona kingine tofauti na hicho.
Kinachofahamika ni kwamba serikali ya Urusi imekanusha kabisakuhusika na madai yanayotolewa na badala yake imewashutumu viongozi wa nchi za Magharibi kwa kuanzisha kampeini ya kutoa taarifa zisizo za kweli kuhusu kinachomsibu kiongozi huyo wa upinzani,bwana Navalny.
Urusi badala yake inasema uchunguzi ulifanywa na madaktari wake ambao walihusika mwanzoni kabisa kumtibu Navalny na majibu ya uchunguzi huo yalionesha hakulishwa sumu. Kisa hiki cha Navalny kimezidisha mivutano kati ya Urusi na nchi za Magharibi na hasa kimeuvuruga kabisa uhusiano na Ujerumani.