NATO yaonya mapigano makali kuwepo Ukraine
25 Juni 2015Stoltenberg amewaambia mawaziri wa ulinzi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya NATO wanaokutana kwa siku ya pili hii leo katika makao makuu ya jumuiya hiyo yaliyoko mjini Brussels kuwa makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwezi Februari mwaka huu mjini Minsk kati ya Ukraine,Urusi, Ujerumani na Ufaransa yanaendelea kukiukwa na kuna uwezekano wa kurejea kwa mapigano makali Ukraine.
Katibu mkuu huyo wa NATO ameongeza kusema Urusi inaendelea kuwaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki mwa Ukraine kwa kuwapa mafunzo, silaha na kuyatuma majeshi yake huku ikiweka idadi kubwa ya vikosi vya majeshi yake katika mpaka na Ukraine.
Makubaliano ya Minsk ndiyo suluhu bora
Stoltenberg amesema nafasi nzuri zaidi ya kufikia amani Ukraine ni kwa kutekelezwa kikamilifu kwa makubaliano ya Minsk na kuzitaka pande zote zinazohusika kuhakikisha utekelezwaji huo hasa Urusi.
Hata hivyo NATO imekanusha mapendekezo yaliyoibuliwa na wanahabari kuwa matamshi hayo ya Stoltenberg kuwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na Urusi kuendelea kuwasaidia waasi hao yanamaanisha makubaliano ya Minsk yamekufa.
Urusi imekanusha kuwa inahusika moja kwa moja katika mzozo huo wa Ukraine ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 6,500 katika kipindi cha miezi kumi na tano tangu uanze mwaka jana.
Nchi 28 wanachama wa NATO wameidhinisha hatua kadha wa kadha kuimarisha ulinzi na kuzihakikishia nchi washirika mashariki mwa Ulaya kuwa zitawaunga mkono dhidi ya kile ilichokitaja NATO kuwa uchokozi wa Urusi barani Ulaya.
Ukraine kupewa msaada na NATO
Mkutano huo wa NATO umetangaza hii leo kuwa baraza la pamoja kati yake na Ukraine lililoundwa kuratibu uhusiano na taifa hilo ambalo si mwanachama wa NATO baada ya kukamilika vita baridi limetathimini juhudi za kuisaidia Ukraine kufanya mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi.
Stoltenberg amesema vita dhidi ya ufisadi ni muhimu hasa kuhakikisha Ukraine inaweza kujisimamia katika kuendesha shughuli zake. NATO pia imekubali kuisaidia Ukraine kusimamia shughuli za kudhibiti usafiri wa angani huku Poland, Norway na Uturuki zikitarajiwa kushirikiana nayo katika kubadilishana taarifa ili kuboresha usalama na usimamizi wa safari za ndege.
Waziri wa ulinzi wa Uingereza Michael Fallon amesema nchi yake inatanua mpango wa kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Ukraine wa kiufundi, kimatibabu na kukusanya taarifa za kijasusi ili kuwasaidia wanajeshi hao kukabiliana na ubabe kutoka Urusi.
Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga