1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yalaani mashambulizi nchini Syria

28 Februari 2020

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg amelaani mashambulizi ya angani yanayofanywa na serikali ya rais Bashar al-Assad na Urusi baada ya wanajeshi 33 wa Uturuki kuuawa katika mkoa wa Idlib.

https://p.dw.com/p/3YaWv
Nato-Generalsekretär Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa NATO, Jens StoltenbergPicha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Mashambulizi hayo yamewauwa wanajeshi 33 wa Uturuki na Ujerumani imeyaita uhalifu wa kivita. 

Mabalozi wa nchi 29 washirika wa Jumuiya ya kujihami ya NATO watakutana leo mjini Brussels  kushauriana kuhusu matukio nchini Syria kufuatia mauaji ya wanajeshi 33 wa Uturuki.

Kikao hicho kinafanyika kufuatia ombi la Uturuki chini ya ibara ya 4 ya mkataba wa Washington ulioiunda jumuiya hiyo.

Msemaji wa Stoltenberg mapema leo amelaani muendelezo wa mashambulizi hayo ya angani yanayowalenga raia jumla kwenye mkoa huo wa Idlib na kutoa mwito kwa serikali ya Syria na mshirika wake Urusi kuacha mashambulizi na kuheshimu sheria ya kimataifa pamoja na kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kupata suluhu ya amani.

Alikuwa akizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, kwa njia ya simu.

Stoltenberg ameziomba pande zinazovutana kupunguza hali ya hatari na kuepusha kudhoofisha hata zaidi hali ya kiutu kwenye eneo hilo.

Umoja wa Ulaya wataka machafuko yakomeshwe

Josep Borrell in Berlin PK
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell Picha: picture-alliance/dpa/A. Hosbas

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ametoa mwito machafuko mkoani Idlib na viunga vyake yakome mara moja akionya kuwa umoja huo utatafakari hatua zote zitakazohitajika kulinda usalama wake.

Takriban wanajeshi 33 wa Uturuki wameuawa kwenye shambulizi la angani lililofanywa na majeshi ya serikali ya Syria mkoani humo, hii ikiwa ni kulingana na maafisa wa Uturuki, idadi ambayo ni kubwa zaidi ya vifo kwa Uturuki kwa siku moja tangu ilipojiingiza kwa mara ya kwanza kwenye mzozo huo wa Syria mwaka 2016.

Gavana wa jimbo la Uturuki la Hatay lililopakana na mkoa wa Idlib, Syria Rahmi Dogan, amesema wanajeshi hao waliuawa na wengine walijeruhiwa vibaya katika shambulizi hilo la jana jioni.

Urusi imekataa kubeba dhamana kwa mashambulizi ya kutokea angani yaliyowaua wanajeshi hao karibu na mji wa Behun katika taarifa ya wizara ya ulinzi iliyotangazwa na shirika la habari la taifa, TASS.

Takribani wanajeshi 50 wa Uturuki tayari wameuawa tangu mwanzoni mwa mwezi Disemba.

Uturuki yaitisha kikao cha dharura

Türkei l Präsident Recep Tayyip Erdogan
Rais Recep Tayyip Erdogan wa UturukiPicha: picture-allliance/AP/B. Ozbilici

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan aliitisha mkutano wa dharura wa kiusalama mjini Ankara, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la serikali, Anadolu.

Msemaji wa Erdogan Ibrahim Kalin, ambaye pia ni afisa mwandamizi kwenye wizara ya mambo ya kigeni, pia amezungumza na mshauri wa masuala ya usalama wa taifa nchini Marekani, Robert O'Brien.

Uturuki leo imeitaka jumuiya ya kimataifa itangaze eneo lisiloruhusiwa ndege kuruka katika anga la mkowa Idlib kaskaszini magharibi mwa nchi hiyo kuwalinda raia kutokana na mashambulizi ya mabomu yanayofanywa na majeshi ya Syria kufuatia kuuliwa wanajeshi wake 33.

Thamani ya hisa katika soko la hisa la Borsa mjini Instanbul imeporomoka kwa asilimia 6 kufuatia kuuliwa kwa wanajeshi hao 33 katika hujuma hiyo iliyofanywa mkaoni Idlib ambapo wanajeshi wengine 32 wamejeruhiwa.

Shambulizi hilo linafanyika siku moja baada ya ujumbe wa Urusi kuwepo mjini Ankara kwa siku mbili kwa mazungumzo na maafisa wa Uturuki kuhusiana na hali ilivyo Idlib, ambako mashambulizi yanayofanywa na serikali yamesababisha maelfu ya raia kukimbilia kwenye mpaka na Uturuki.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amelaani mashambulizi dhidi ya raia kwenye mkoa huo na kuyaita ni uhalifu wa kivita.

Kwenye mkutano mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, Maas amesema serikali ya Syria pamoja na mshirika wake Urusi wana wajibu wa kuwalinda raia, lakini badala yake wanashambulia miundombinu yao kama hospitali na shule. Ametoa mwito wa kuchukuliwa hatua kwa wahusika wa mzozo huo.