1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yakiri imelikosea lengo lake na kupiga wanakoishi raia

20 Juni 2011

Jumuia ya NATO imekiri "dosari mbili" zimetokea nchini Libya katika kipindi cha masaa 24: hujuma za mabomu yaliyogharimu maisha ya raia mjini Tripoli na nyengine dhidi ya vikosi vya waasi.

https://p.dw.com/p/11fU6
Askari wa zima moto na raia wa kawaida wanasaidia kukufukua katika jengo moja lililohujumiwa kwa mabomu ya NATO nje ya mji mkuu TripoliPicha: AP

Hujuma za NATO za jumamosi kuamkia jumapili mjini Tripoli zimegharimu maisha ya watu tisa-watano kati yao ni wa familia moja.Watu wengine 18 wamejeruhiwa-hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Libya-Moussa Ibrahim.

Katika taarifa yake,jumuia ya kujihami ya NATO imekiri hujuma zake katika mji mkuu wa Libya zimegharimu maisha ya raia wa kawaida.Hii ni mara ya kwanza kwa jumuia ya kujihami ya NATO kukiri " dosari zilizogharimu maisha ya raia wa kawaida":Msemaji wa opereshini za kijeshi za NATO nchini Libya,luteni kanali Mike Bracken anasema:

"Kituo cha makombora ndicho kilichokuwa kimelengwa katika hujuma hizo za jumamosi usiku mjini Tripoli.Lakini yadhihirika lengo moja lililowekwa halijafikiwa kutokana na makosa katika mtambo wa kufyetulia silaha.Kosa hilo la kiufundi huenda limesababisha hasara ya maisha ya watu kadhaa.Nato inasikitika na inajitahidi sana katika hujuma zake dhidi ya utawala unaotumia nguvu dhidi ya raia wake ."

NATO Verteidigungsminister Brüssel Belgien Treffen
Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO Anders Fogh RasmussenPicha: AP

Msemaji wa serikali ya Libya Mussa Ibrahim anailaumu jumuia ya NATO kufanya vitemndo vya "kinyama kwa kuwalenga makusudi raia."

Hujuma 1500 zimeshafanywa na NATO tangu ilipokabidhiwa uongozi wa opereshini za kijeshi dhidi ya utawala wa Muammar Gaddafi zilipoanza March 31 mwaka huu.

Tangazo la "kosa hilo" limetolewa saa 24 baada ya jumuia ya kujihami ya NATO kukiri imehujumu "kwa makosa" mlolongo wa magari ya vikosi vya waasi katika eneo la Brega,June 16 iliyopita.Matukio yasiyopungua maweili ya aina hiyo yamewahi kutokea pia siku za nyuma.

Flüchtlinge aus Libyen an der tunesisch libyschen Grenze
Mikururo ya watu wanaokimbia mapigano nchini LibyaPicha: AP

Taarifa hizi mbili zimetolewa katika wakati mgumu,miezi mitatu baada ya opereshini hizo kuanza.Ili kuepukana na balaa la kuzidi makali mzozo wa Libya,maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa mataifa,Umoja wa Ulaya,jumuia ya nchi za kiarabu,jumuia ya nchi za kiislam na Umoja wa Afrika wamekutana mjini Cairo jumamosi iliyopita na kuzungumzia umuhimu wa kupatikana ufumbuzi wa kisiasa kwa mzozo wa Libya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/reuters,afp

Mhariri:Yusuf Saumu