NATO yakanusha tena kutaka kumuua Gaddafi
11 Mei 2011Asubuhi ya leo (11.05.2011) kwa kipindi cha karibuni saa nzima, sehemu ya mashariki ya Tripoli ilishuhudia makombora ya mfululizo huku ndege za NATO zikiranda angani.
Shahidi mmoja ameliambia Shirika la Habari la AFP kuwa miripuko ilianza kuonekana kuanzia saa 1:30 hadi 2:15 asubuhi.
NATO inasema kwamba tangu ichukuwe operesheni hii kutoka mikononi mwa majeshi ya Marekani, Uingereza na Ufaransa, mnamo mwisho wa mwezi Machi, ndege zake zimeshambulia mara 6,000 kwa namna mbali mbali yakiwemo zaidi ya 2,000 ya makombora.
Lakini wakosoaji wa operesheni hii wamekuwa wakisema kuwa NATO inakusudia kumuua Gaddafi, kwani mara kadhaa imelenga makaazi yake au familia yake.
Hata hivyo, akizungumza kutokea kituo cha kuendeshea operesheni cha NATO kilichoko mjini Naples, Italia, Brigedia Jenerali Claudio Gabellini, amesema kwamba Jumuiya yake inalenga vituo vya kijeshi tu na sio watu binafsi.
"Hatumlengi mtu. Sehemu tunazozipiga, kama hizi za leo asubuhi, zilikuwa na mahandaki na vituo vya kuongezea vita vya jeshi la Libya." Amesema Brigedia Jenerali Gabellini katika ujumbe wake kwa njia ya video kupitia mtandao.
Lakini Waziri wa Ulinzi wa Italia, Ignazio La Russa, amekwenda umbali wa kusema kwamba, kama Kanali Gaddafi akijiweka kwenye vituo vya kijeshi vinavyoshambuliwa, basi naye atakuwa ni mlengwa halali wa mashambulizi ya NATO.
"Ikiwa amri za mashambulizi dhidi ya raia zinatolewa kutoka vituo vinavyoshambuliwa na NATO, naye Gaddafi akakutikana kwenye vituo hivyo, anakuwa moja kwa moja sehemu ya wanaostahiki kushambuliwa." La Russa amesema katika mahojiano yaliyochapishwa leo na gazeti moja nchini Italia.
Waasi wadai kusonga mbele
Katika hatua nyengine, waasi wamesema kwamba wamevirudisha nyuma vikosi vya Gaddafi kutoka upande wa magharibi wa bandari ya Misrata, ambao ulikuwa chini ya udhibiti wa wanajeshi wa Gaddafi kwa miezi miwili sasa.
Baada ya mapigano makali, waasi hao waliweza kuudhibiti upande wa fukwe za Misrata na hivyo kuwawezesha maelfu ya watu waliokwama, kuweza kuondoka kwenye mji huo uliogeuzwa medani ya mapambano.
Waasi wamewasukuma wanajeshi wa Gaddafi umbali wa kilomita zipatazo 15 kutoka Misrata kuelekea mji wa Dafina, na sasa wanajitayarisha kuelekea mji wa Zliten, ambao ni mji mwengine mkubwa katika barabara ya kuelekea Tripoli.
Kamanda mmoja wa waasi, Haj Mohammed, ameliambia Shirika la Habari la Reuters, kwamba kila siku wanapiga hatua fulani kuelekea Tripoli, na kwamba hakuna la kuwazuia hadi ushindi. Hata hivyo, madai haya ya ushindi hayajaweza kuthibitishwa na vyanzo vilivyo huru.
Umoja wa Ulaya kufungua ofisi Benghazi
Katika hatua nyengine, Umoja wa Ulaya unapanga kufungua ofisi yake katika mji unaodhibitiwa na waasi wa Benghazi ili kuratibu misaada kwa baraza la kitaifa la mpito, linaloongozwa na waasi hao.
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja huo, Catherine Ashton, ameliambia Bunge la Ulaya linalokutana leo hii mjini Strasbourg, Ufaransa, kwamba ofisi hiyo itauwezesha Umoja wa Ulaya kuwa karibu na watu wa Libya, kujadiliana nao na kuwasaidia kuimarisha usalama na taasisi za kijamii na za kisiasa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji