NATO yakanusha kuwa tishio kwa Urusi
27 Desemba 2014Msemaji wa jumuiya ya NATO Oana Lungescu amesema mjini Brussels Ijumaa usiku (26.12.2014) kwamba hatua zozote zile zinazochukuliwa na NATO kuhakikisha usalama wa nchi wanachama wake huwa dhahiri kwa ajili ya kujihami, zinakuwa za kiwango kinachostahiki na zinazozingatia sheria ya kimataifa.
Ameongeza kusema ukweli ni kwamba hatua za Urusi zikiwemo zile za hivi sasa nchini Ukraine ndio zenye kuvunja sheria ya kimataifa na kudhoofisha usalama barani Ulaya.
Amekaririwa akisema "NATO itaendelea kutaka kuwa na ushirikiano wenye tija na Urusi" lakini hilo litawezekana tu kwa Urusi kuzingatia sheria na misingi ya kimataifa ikiwemo haki kwa mataifa kujiamuliwa kwa hiari yao mustakbali wao.
Waraka mpya wa kijeshi
Waraka wa kanuni mpya ya usalama ya Urusi ambao umechapishwa kwenye mtandao wa Ikulu ya Urusi baada ya kuidhinishwa na Rais Vladimir Putin umeorodhesha mambo 14 iliyoyataja kuwa hatari kwa usalama wa Urusi, jambo la kwanza likiwa ni kutanuka kwa uwezo wa kijeshi wa NATO na kujitanuwa kwa jumuiya hiyo ya mataifa magharibi kwa kuyajumuisha mataifa ya Ulaya mashariki.
Pia mfumo wa Marekani wenye kukusudia kufanya shambulio maalum la kijeshi kwa silaha za kawaida kwa haraka katika muda usiozidi saa moja mahala popote pale duniani, mpango ambao unajulikana kwa jina la "Prompt Global Strike" pia umejumuishwa kwenye waraka huo kuwa ni tishio kwa Urusi.
Mpango huo umetajwa kuwa tishio nambari mbili pamoja na mfumo wa makombora ya kujihami barani Ulaya ambao kwa muda mrefu umekuwa ukishutumiwa na Urusi kama ni tishio kwa uwiano wa kimkakati barani Ulaya.
Matumizi ya silaha za nyuklia
Waraka huo umebakisha vifungu vilivyopita vya kanuni iliyotolewa mwaka 2010 kuhusiana na matumizi ya silaha za nyuklia.
Umesema Urusi inaweza kutumia silaha za nyuklia katika kulipiza kisasi kwa matumizi ya silaha za nyuklia au silaha nyengine zozote za maangamizi makubwa dhidi ya nchi hiyo na washirika wake na pia wakati wa uvamizi wenye kuhusisha matumizi ya silaha za kawaida ambao unatishia uhai wa taifa la Urusi.
Lakini kwa mara ya kwanza kanuni hiyo mpya imesema Urusi inaweza kutumia silaha zinazolengwa kwa matumizi maalum kama sehemu ya mkakati wa kujihami. Waraka huo haukusema wakati gani na vipi nchi hiyo inaweza kufikia uamuzi wa kutumia silaha hizo ambazo zinajumuisha makombora yanayofyatuliwa ardhini kwa ajili ya kushambulia maeneo ya nchi kavu,makombora yanayofyatuliwa kutoka angani na kwenye nyambizi halikadhalika mabomu na mizinga yenye kuelekezwa shabaha zake.
Uhusiano wadhoofika
Uhusiano wa Urusi na mataifa ya magharibi umeathirika sana kuwahi kushuhudiwa tokea nyakati za Vita Baridi na NATO ilivunja uhusiano wake na Urusi baada ya nchi hiyo kuinyakuwa Rasi ya Crimea kutoka Ukraine hapo mwezi wa Machi. Ukraine na mataifa ya magharibi pia yamekuwa yakiishutumu Urusi kwa kuuchochea uasi mashariki mwa Ukraine kwa kupeleka wanajeshi wake na silaha madai ambayo Urusi imeyakanusha.
Rais wa zamani wa Urusi Mikhail Gorbachev ambaye huko nyuma alikuwa akimkosoa Putin hapo Ijumaa ameiunga mkono kwa nguvu serikali ya Urusi katika mzozo wake na mataifa ya magharibi kwa kusema kwamba hatua inazochukuliwa na Urusi zinatokana na hatua zinazochukuliwa na Marekani na NATO.
Amekaririwa akisema anafikiri kwa kiasi kikubwa rais yuko sahihi wakati alipoiwajibisha Marekani katika mzozo huo.
Marekani na Umoja wa Ulaya zimeiwekea Urusi vikwazo ambavyo vimezidi kuzorotesha uchumi wa Urusi na kuchangia kushuka sana kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo ruble ambayo imepoteza nusu ya thamani yake mwaka huu.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AP/dpa
Mhariri: Elizabeth Shoo