1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yaidhinisha mkakati mpya kwa miaka 10

Kabogo Grace Patricia20 Novemba 2010

Mkakati huo umeidhinishwa na viongozi wa Jumuiya ya kujihami ya NATO katika mkutano wao wa Lisbon, Ureno.

https://p.dw.com/p/QE8X
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen.Picha: AP

Viongozi wa jumuiya ya kujihami ya NATO, wameidhinisha mkakati mpya kwa miaka kumi ijayo kuruhusu muungano huo wa kijeshi kukabiliana na vitisho vipya vya kigaidi, ikiwemo mashambulio katika mtandao wa internet. Mkakati huo umeidhinishwa katika mkutano wao mjini Lisbon, Ureno, ambapo pia wamekubaliana kuanzisha ulinzi wa pamoja dhidi ya makombora, hata pamoja na Urusi.

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, akiwasilisha waraka wenye kurasa 11, alisema mataifa yote 28 wanachama yameuidhinisha mkakati huo. Ameelezea hatua hiyo kama ya kihistoria.

Rais Barack Obama wa Marekani, amesema ulinzi dhidi ya makombora utakuwa imara kuyalinda mataifa yote wanachama wa NATO barani Ulaya. Marekani inatengeneza makombora ya masafa marefu yatakayokuwa kinga dhidi ya makombora ya adui, ambayo yatapelekwa Ulaya na kuunganishwa na mifumo kadhaa ya masafa mafupi ya mataifa mengine wanachama.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema mkakati huo uko wazi na unaoeleweka. Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev leo atahudhuria mkutano huo wa NATO mjini Lisbon. Mkutano huo pia utatafuta mkakati wa kuviondoa vikosi vya NATO nchini Afghanistan vinavyomaliza muda wake wa mapambano mwishoni mwa mwaka 2014.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE,RTRE,AFPE)

Mhariri: Sekione Kitojo