1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nato yaendelea kushambulia Libya

Saumu Ramadhani Yusuf7 Juni 2011

p>Mashambulizi zaidi ya angani yameendelea kuutikisa mji mkuu wa Libya Tripoli mchana wa leo.Mashambulio hayo yamekuja baada ya katibu mkuu wa NATO hapo jana kusema kwamba enzi ya Gaddafi imeshamalizika.

https://p.dw.com/p/11W21
Helikopta za Nato zaendelea kushambulia TripoliPicha: picture-alliance/dpa
Urusi inaendelea na juhudi zake za kutafuta njia ya kulipatia ufumbuzi suala la Libya ambalo hadi sasa ni Kitendawili kutokana na ukaidi wa kukataa kuondoka madarakani Kanali Muammar Gaddafi.

Mfululizo wa mashambulizi ya angani umeshuhudiwa kutikisa kitovu cha mji mkuu wa Libya Tripoli na kuacha moshi ukitanda katika anga yote ya mji huo ambako ndiko kuliko na makao ya kiongozi wa Taifa Kanali Muammar Gaddafi.Mwandishi wa habari wa shirika la habari la Ufaransa AFP anasema mripuko wa kwanza ulishuhudiwa saa 10 na 45 kwa saa za Tripoli na kufuatia na mashambulio mengine 7 ya mabomu kutoka angani.Msemaji wa Serikali Mussa Ibrahim amewaambia waandishi wa habari kwamba watu wengi wamejeruhiwa bila ya kutoa taarifa zaidi. Makaazi ya eneo hilo ikiwemo ya Kanali Gaddafi yamekuwa yakilengwa mara kwa mara na Opresheni ya angani ya vikosi vya NATO.Katibu mkuu wa jumuiya hiyo ya Kujihami akizungumza na waandishi wa habari mjini Brussels katika makao makuu ya jumuiya hiyo alisema ''Ujumbe wa Nato kwa Walibya uko wazi.Nato na washirika wake wanawalinda raia.Ujumbe wa Nato kwa Utawala wa Gaddafi,ni kwamba Tulianzisha opresheni hii na tutaikamilisha.''

NO FLASH NATO Angriff Tripolis Libyen
Mfululizo wa miripuko ya mabomu ya Nato yameutikisa mji wa Tripoli,na moshi kugubika anga nzima ya mji huoPicha: picture alliance/dpa

Na Umoja wa Ulaya umekubaliana kuziweka bandari nyingine sita za Libya katika orodha ya maeneo yaliyowekewa Vikwazo yanayosimamiwa na serikali ya Muammar Gaddafi.

Na upande mwingine serikali ya China leo nayo imesema kwamba wanadiplomasia wake wameshawasili mjini Benghazi kukutana na wanachama wa upinzani na pia kutathmini hali ya mzozo huo katika taifa hilo lenye utajiri wa mafuta.Wanadiplomasia hao wakitokea katika ofisi za ubalozi wa China nchini Misri wamekusudia zaidi kutafuta mwafaka kuhusiana na suala la hali ya kibinadamu pamoja na hali ya wawekezaji wa China katika taifa hilo la Libya.Urusi pia imeshamtuma mjumbe wake katika taifa hilo ambaye hii leo amekutana na viongozi wa waasi ikiwa ni ziara ya kwanza tangu kuwahi kufanywa na afisa wa ngazi ya juu kutoka Urusi.Nia ya mjumbe huyo wa Urusi Mikhail Margelov ni kusimamia mazungumzo kati ya kambi mbili zinazohasimiana.Urusi na China zote zikiwa ni wanachama wa kudumu kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa zilijizuia kupiga kura juu ya azimio la Umoja huo lililotoa nafasi ya kuchukuliwa hatua ya kijeshi dhidi ya Libya.Uhispania nayo imetangaza kumpeleka waziri wake wa mambo ya nje Benghazi kukutana na waasi.Mauritania imetoa msimamo wake kuhusu Libya ikisema Kanali Moamer Gaddafi hawezi tena kuiongoza Libya na inambidi aachie madaraka.

FLASH-GALERIE Muammar al-Gaddafi
Kanali Gaddafi atoa ukanda wa sauti akisisitiza haondoki madarakani wala nchini LibyaPicha: picture alliance/dpa

Lakini pia rais Ould Abdel Aziz wa Mauritania anayeongoza jopo la viongozi wa Umoja wa Afrika wanaohusika katika kutafuta suluhisho la mgogoro wa Libya ameongeza kusema kwamba  anatilia shaka umuhimu wa mashambulio ya angani ya Vikosi vya Nato.

Mwandishi Saumu Mwasimba/APE/AFPE

Mhariri AbdulRahman.