1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO na operesheni za kijeshi Libya

15 Aprili 2011

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen, amesema kwamba kuna ishara kwamba mataifa yanayounda muungano huo, yatatoa ndege zaidi za kivita zinazohitajika katika operesheni ya Libya.

https://p.dw.com/p/10uT5
Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh RasmussenPicha: AP

Ameyasema hayo leo wakati majeshi la Libya yamefanya mashambulio mapya katika mji wa Misrata na pia kuwashambulia waasi katika mji wa Ajdabiyah ulioko mashariki mwa Libya.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku mbili na mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa jumuiya ya NATO, katibu mkuu wa jumuiya hiyo Anders Fogh Rasmussen amesema hajapokea ombi rasmi kuhusu ndege zaidi zinazohitajika kwa ajili ya operesheni hiyo nchini Libya, lakini anatarajia kuongezwa kwa ndege zaidi za vita hivi karibuni.

Awali kamanda wa jeshi la NATO alisema kuwa muungano huo unahitaji ndege zaidi kwa ajili ya kulishambulia jeshi la Gaddafi na wakati huo huo kujiepusha kushambulia raia.

Hata hivyo nchi hizo za jumuiya ya NATO zimekuwa zikitofautiana pia na juu ya kuimarisha hatua za kijeshi dhidi ya vikosi vya Gaddafi.

Wakati Uingereza na Ufaransa zikiwataka wanachama kutoa ndege zaidi za kivita, baadhi ya nchi zikitaka hatua zaidi za kijeshi, Italia imesema leo kwamba ndege zake za kijeshi hazitoshiriki katika mashambulio nchini Libya na kwamba nchi hiyo inafanya vya kutosha kuunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa kuyalinda maisha ya raia.

Hayo yamesemwa na Waziri mkuu wa nchi hiyo Silvio Berlusconi wakati alipokuwa akizungumza na wabunge mjini Roma, uamuzi ambao ulisisitizwa pia na Waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Ignazio La Russa, akisema kuwa tayari wameshafanya mengi ya kutosha.

Wakati wanachama wa jumuiya ya NATO wakijadiliana mjini Berlin hapa Ujerumani, majeshi ya serikali ya Libya yamefanya mashambulio katika mji wa Misrata hii leo huku watu wanane wakiripotiwa kufa na wengine saba wamejeruhiwa.

Majeshi ya Gaddafi pia yamewashambulia waasi na kumuua mmoja katika mji wa mashariki wa Ajdabiyah.

Katika hatua nyingine, meli iliyowabeba wahamiaji kutoka nchi za Afrika na Asia ambao wengi wakiwa katika hali mbaya kutokana na uhaba wa maji na chakula, imeondoka leo asubuhi kutoka katika mji wa Misrata kuelekea Benghazi.

Msemaji wa shirika la kimataifa la uhamiaji, Jemini Pandya amesema meli hiyo ilifanikiwa kupakua tani mia nne za misaada usiku mzima licha ya mashambulio ya jana mjini humo.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters, afp,dpa)

Mhariri:Josephat Charo