NATO kutekeleza marufuku ya ndege kuruka kwenye anga ya Libya
25 Machi 2011Lakini, makubaliano hayo hayaipi NATO jukumu kamili la kusimamia operesheni zote za kijeshi. Baada ya siku sita za majadiliano miongoni mwa mabalozi wa mataifa 28 wanachama wa NATO, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Anders Fogh Rasmussen amesema hadi wanasiasa watakapokubali kuipa NATO jukumu zima la kusimamia shughuli zote za kijeshi, kimsingi kutakuwa na wasimamizi wawili.
Maafisa wa NATO wamesema kuwa uamuzi unatarajiwa kutolewa keshokutwa Jumapili, kuhusu iwapo kuiongeza jumuiya hiyo mamlaka ya kusimamia operesheni zote za kijeshi. Hatua hiyo itajumuisha mashambulizi dhidi ya vikosi vya jeshi la nchi kavu vya Kanali Gaddafi ambavyo vinashambulia maeneo ya raia.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema hakuna dalili kuwa serikali ya kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi ilikuwa inatekeleza matakwa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kusimamisha mara moja mapigano. Amesema baraza hilo huenda likachukua hatua zaidi iwapo Libya itaendelea kuyapuuza matakwa hayo.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza, William Hague amesema vurugu zinaendelea kufanywa dhidi ya raia wa Libya. Ndege za mataifa ya Magharibi jana zilishambulia katika maeneo ya Tripoli wakati ambapo operesheni yao imeingia usiku wa sita, huku vifaru vya serikali vikiingia tena kwenye mji wa tatu kwa ukubwa wa Misrata.
Katika mji huo, vifaru hivyo viliizingira hospitali kuu na kukata mawasiliano ya bandari hivyo kuwafanya maelfu ya watu kutoka Misri na maeneo mengi ya nchi za Ulaya kukwama. Meli mbili za kivita za Libya pia zimepiga doria nje ya bandari hiyo. Kuna taarifa kwamba kuna mapigano makali katika eneo la mashariki kwenye mji wa Ajdabiyah.