NATO kujadili kudunguliwa kwa ndege ya Uturuki
25 Juni 2012Baraza la mawaziri la Uturuki linatarajiwa kukutana leo (25.06.2012) kujadili tukio hilo la Ijumaa iliyopita, ambalo yumkini likabadili mtazamo wa jumuiya ya kimataifa kuhusu maandamano ya mapinduzi dhidi ya rais wa Syria, Bashar al Assad yaliyodumu miezi 16 sasa.
Jumuiya ya kujihami ya NATO imesema itakutana kesho kujadili dai la Uturuki kwamba Syria iliidungua ndege yake ya kivita katika anga ya kimataifa na wala sio ndani ya anga ya Syria kama utawala wa rais Asad unavyodai. NATO imesema itafanya kikao cha dharura kufuatia ombi la Uturuki iliyotumia ibara ya nne ya mkataba ulioiunda jumuiya hiyo, inayojumuisha vitisho vya usalama dhidi ya nchi wanachama.
Msimamo wa Uturuki wapongezwa
Magazeti ya Uturuki yameipongeza hatua ya waziri mkuu wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdogan, kutumia ibara hiyo ya mkataba wa NATO unaotaka kufanyike mashauriano ya dharura kama nchi mwanachana inahisi masilahi yake ya usalama yako hatarini. "Uturuki imechukua hatua" ndivyo yalivyoandika magazeti ya Milliyet na Vatan katika vichwa vyao vya habari chini ya bendera ya jumuiya ya NATO. Mwandishi wa makala wa gazeti la Sabah, Mehmet Barlas alisema baadhi ya Waturuki wanaliona shambulizi la Ijumaa iliyopita kama tangazo la vita la Syria.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, ameiambia televisheni ya TRT nchini humo kwamba ndege hiyo ilikuwa katika anga ya kimataifa wakati ilipodunguliwa. Aliongeza kuwa Syria haikutoa onyo lolote kabla kuishambulia ndege hiyo iliyokuwa ikifanya mazoezi kuufanyia majaribio mfumo wa rada ya Uturuki. Mpaka sasa marubani wote wawili wa ndege hiyo hawajulikani waliko.
Hisia kali zaibuka
Syria imekiri kuidungua ndege hiyo ya Uturuki aina ya F-4 Phantom, lakini inasisitiza iliitambua kuwa ya Uturuki baada ya kuiangusha. Msemaji wa serikali ya Syria, Jihad Makdissi, aliliambia gazeti la serikali la Al-Watan kwamba kilichotokea ni ajali na wala si shambulizi kama baadhi wanavyopenda kuliita.
Lakini Uingereza imeuonya utawala wa rais Assad kutofanya kosa la kuamini unaweza kufanya utakavyo bila kuadhibiwa. Imeliita shambulizi hilo lililofanywa mashariki mwa bahari ya Mediterania kuwa ni kitendo cha kikatili na imesema iko tayari kuunga mkono hatua kali katika Umoja wa Mataifa. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza, William Hague, amesema Syria itabebeshwa dhamana kwa tabia yake.
Akizungumza kuhusu shambulizi hilo akiwa ziarani nchini Bangladesh, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, alisema, "Nataka kisa hiki kichunguzwe kikamilifu. Napongeza hatua ya Uturuki kuwa na utulivu. Kila kitu lazima kifanyike ili kuzuia kuongezeka kwa hali ya wasiwasi katika eneo hilo."
Naye waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, ameliita shambulizi hilo kuwa la makusudi na lisilokubalika. Katika taarifa yake Clinton alisema tukio hilo linaonyesha jinsi utawala wa Syria usivyojali sheria za kimataifa, maisha ya binaadamu, amani na usalama
Italia, mwanachama mwengine wa NATO, imeilaani Syria kwa shambulizi hilo. Waziri wa mambo ya kigeni wa Italia, Giulio Terzi, amesema watashiriki kikamilifu kwenye mkutano wa NATO hapo kesho.
Duru za serikali ya Uhispania zimesema mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya watalijadili shambulizi hilo kwenye mkutano wao mjini Luxembourg hii leo.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE
Mhariri: Hamidou, Ummilkheir