1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO kufanya mazoezi makubwa kabisa Ujerumani

11 Juni 2023

Nchi washirika wa NATO zinapanga kuendesha mazoezi ya kijeshi kwenye anga ya Ujerumani. Maeneo matatu yatafungwa kwa muda. Safari za ndege za kiraia hazitaruhusiwa katika anga ambapo mazoezi hayo yatakuwa yanaendela.

https://p.dw.com/p/4SRZS
 NATO-Manöver | Air Defender 23
Picha: Jane Schmidt/Bundeswehr

Jumuiya ya kijeshi ya NATO inapanga kuendesha mazoezi ya kijeshi kwenye anga ya Ujerumani. Maeneo matatu yatafungwa kwa muda na hivyo safari za ndege za kiraia hazitaruhusiwa katika maeneo hayo hali ambayo itasababisha kucheleweshwa kwa baadhi ya safari za ndege zinazotarajiwa kuruka katika anga ambapo mazoezi hayo yatakuwa yanaendela.

Baadhi ya ndege za kivita zitakazotumika kwenye mazoezi ya kijeshi ya NATO.
Baadhi ya ndege za kivita zitakazotumika kwenye mazoezi ya kijeshi ya NATO.Picha: Falk Bärwald/Bundeswehr

Kuanzia Jumatatu tarehe12 hadi tarehe 23 Juni, nchi 25 wanachama wa NATO zitashiriki katika mazoezi hayo. Takriban ndege 250 zitawekwa katika kambi sita za kijeshi. Marekani itapeleka ndege 100 katika Bahari ya Atlantiki.

Wanajeshi wa nchi wanachama wa jumuiya ya kijeshi ya NATO watapokea mafunzo katika anga tatu za Ujerumani, kwenye bahari ya kaskazini, eneo la mashariki mwa Ujerumani na katika ukanda mdogo wa kusini mwa Ujerumani.

Katikati: Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na wanajeshi wa Ujerumani.
Katikati: Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na wanajeshi wa Ujerumani.Picha: Mindaugas Kulbis/AP/dpa/picture alliance

Maeneo ya anga yaliyoteuliwa kwa ajili ya  mazoezi yatafungwa kila siku kwa saa kadhaa kuanzia hiyo tarehe 12 hadi tarehe 23 Juni na hivyo ndege za kiraia hazitaruhusiwa kufanya safari zake za kawaida katika muda ambapo anga itakuwa imefunwa kwa ajili ya mazoezi ya kijeshi.

Mafunzo hayo yatahusu kukabiliana na nyakati za matatizo.

Jeshi la Wanahewa la Ujerumani limekuwa linakabiliwa na changamoto kubwa kwa miongo kadhaa na baada ya miaka minne ya maandalizi,mazoezi hayo ya kijeshi yaliyopewa jina la NATO Air Defender 23, yanatarajiwa kuwa makubwa zaidi na ya aina yake tangu muungano huo wa kijeshi ulipoanzishwa mnamo mwaka 1949, ambapo Ujerumani ndio mwenyeji na wakati huohuo itakuwa ndio mahala pa kuhifadhia vifaa na usimamizi wa usafirishaji wa vifaa hivyo.

NATO inatoa ujumbe kuwa iko imara

Mtaalamu wa Taasisi ya Ujerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama, Torben Arnold, amesema jumuiya ya kujihami ya NATO inataka kutoa ujumbe wa kisiasa kwa kufanya mazoezi haya ya Ulinzi wa Anga, ameiambia DW kwamba bila shaka, hii ni ishara ya wazi, inayoashiria kwamba ingawa anga ya Ulaya ina shughuli nyingi, lakini wanachama wa NATO wako tayari kulinda kila sentimita ya eneo la nchi wanachama wa NATO.

Kifaru cha Norway aina ya CV90 -, baharini kuna manowari mbili za kijeshi aina ya Mark ll.
Kifaru cha Norway aina ya CV90, baharini kuna manowari mbili za kijeshi aina ya Mark ll.Picha: Marco Dorow/Bundeswehr/dpa/picture alliance

Zaidi ya wanajeshi 10,000 kutoka nchi za NATO watashiriki katika mazoezi kadhaa. Luteni Jenerali Gerhartz wa Jeshi la Wanahewa la Ujerumani amesema mazoezi kama haya yaliongezwa kwenye ratiba baada ya machafuko katika uwanja wa ndege wa Kabul mnamo mwaka 2021 wakati Marekani na washirika wake walipokatiza misheni yao nchini Afghanistan.

Mazoezi mengine ni pamoja na namna ya kuwasaidia wanajeshi wa ardhini kutokea angani, mapigano ya angani dhidi ya ndege za adui na jinsi ya kuzuia makombora ya masafa ya kati kwa kutumia ndege za kivita za NATO.

Vikosi vya Marekani vitaleta ndege za kivita za kisasa zaidi aina ya F-35 kushiriki mkwenye mazoezi hayo. Katika bahari ya kaskazini mwa Ujerumani yatafanyika mazoezi ya kujilinda dhidi ya manowari au meli za adui.

Manowari ya kijeshi ya Ujerumani inayoitwa Bayern ikikata mawimbi pembezoni mwa pwani ya Lebanon tarehe 29.02.2018.
Manowari ya kijeshi ya Ujerumani inayoitwa Bayern ikikata mawimbi pembezoni mwa pwani ya Lebanon tarehe 29.02.2018.Picha: Michael Kappeler/AFP/Getty Images

Sio siri kwamba linapokuja suala la "adui", wengi barani Ulaya kwanza hufikiria Urusi na uvamizi wake dhidi ya Ukraine tangu Februari 24, mwaka 2022. Lakini, wakati akiwasilisha mipango ya mazoezi ya Air Defender 23 kwa vyombo vya habari huko mjini Berlin mnamo Juni 7, Luteni Jenerali Gerhartz hakuitaja Urusi hata mara moja.

Balozi wa Marekani nchini Ujerumani, Amy Gutmann, amesema mazoezi hayo yataonyesha uwezo na weledi wa kikosi cha washirika wa NATO kilichofunzwa kujibu kwa haraka na kushughulikia maswala ya dharura.