NATO kuanzisha mazungumzo ya ngazi za juu na Urusi
6 Machi 2009Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Urusi kuivamia Georgia Agosti mwaka jana Urusi kwa upande wake imefurahishwa na taarifa hizo.
Baada ya kuondokana na pingamizi ya Lithuania, mawaziri hao wa mambo ya nchi za nje wa Nato walikubaliana kuanzisha tena mazungumzo ya kile kinachoitwa Baraza la pamoja la Nato na Urusi, baada ya mkutano wa kilele wa nato tarehe 3 na 4 mwezi ujao wa Aprili.
AFPE
Katibu mkuu wa NATO Jaap de Hoop Scheffer alitangaza uamuzi huo lakini hakutaja tarehe wala mahala ambapo mazungumzo hayo yataanzishwa upya zaidi ya kusema tu kwamba yatafanyika hivi karibuni, huenda yakafungamana ana sherehe ya miaka 60 tangu kuanzishwa jumuiya hiyo ya kujihami katika mji wa Strasbourg Ufaransa na mji jirani wa Kehl nchini Ujerumani.
Pamoja na hayo imefahanika kwamba mkutano wa pande hizo mbili katika ngazi kamili ya mabalozi utafanyika mara tuu baada ya mkutano wa viongozi wakuu wa NATO.
Mazungumzo baina ya Nato na Urusi yalisimamishwa mwezi Agosti baada ya Urusi kutuma majeshi katika Jamhuri ya Georgia. Hata hivyo mbali na hatua hiyo mpya, katibu mkuu wa NATO alieleza wazi kwamba bado kuna nyanja kadhaa ambapo pande hizo zina tafautiana na anafikiria kuna maeneo ambamo Urusi inaweza kubali maoni.
Akataja hasa juu ya hatua ya Urusi inayolaaniwa na wengi ya kuyatambua maeneo mawili ya Georgia yaliojitenga-Abkhazia na Ossetia kusini pamoja na mipango yake ya kuweka vituo vya kijeshi katika mikoa hiyo.
Katika hatua ya kuondoa wasi wasi ilizonazo Georgia na Ukraine , ambazo zote zina azimia kujiunga na jumuiya ya NATO huku Urusi ikipinga vikali, mawaziri hao wa mambo ya nchi za nje walikutana na waakilishi wa Georgia na Ukraine.
Katibu mkuzu Scheffer pia alisisitiza kwamba Urusi ni mshirika muhimu katika suala la kuyapa msaada wa mikakati majeshi ya Nato yalioko Afghanistan na pia katika kupambana na ugaidi , madawa ya kulevya na kutapakaa kwa silaha za nuklea.
Itakumbukwa mnamo siku ya Jumanne Rais wa Marekani barack Obama, alifichua kwamba ametuma barua ndefu kwa Rais Dmitry Medvedev wa Urusi, katika jitihada za kutafuta ushirikiano wa pamoja kuhusiana na suala tete la mpango wa nuklea wa iran na mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora uliokua ukipigiwa upatu na utawala wa zamani wa George W.Bush. Hatua hiyo ni dalili ya kutaka kuwepo na ushirikiano mpya utakaoondoa mvutano kati ya Marekani na Urusi. Akisisitiza hilo, waziri wa nje wa Marekani Hillary Clinton alisema mjini Brussels kuwa hii ni nafasi ya kufungua ukurasa mpya.
Bibi Clinton anatarajiwa kukutana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov hii leo, ukiwa wa kwanza kati ya mawaziri hao wawili tangu Rais Obama na utawala wake kuanza kazi mwezi Januari.