1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO, EU na G7 zasimama pamoja kupinga uvamizi wa Urusi

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
24 Machi 2022

Jumuiya ya kujihami ya NATO, Umoja wa Ulaya na kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7 zasema Urusi italipa gharama kubwa kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/48zd1
Belgien | Nato-Sondergipfel zum Ukraine-Konflikt
Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Viongozi wa nchi wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO wamekutana mjini Brussels kwa ajili ya mkutano wa kilele usio wa kawaida kushughulikia hatua za kujibu uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Adam Schultz/picture alliance/ZUMAPRESS

Rais wa Marekani, Joe Biden amesisitiza msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine, huku Uingereza ikijiandaa kuweka vikwazo vipya dhidi ya Urusi. NATO imesema itapeleka wanajeshi zaidi katika nchi wanachama upande wa Ulaya Mashariki.

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema baada ya mkutano wa kilele usio wa kawaida wa viongozi wa NATO kwamba jumuiya hiyo imeweka tayari ulinzi dhidi ya silaha za kemikali na za nyuklia kwa ajili ya kuzilinda nchi wanachama kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg Picha: Johanna Geron/REUTERS

Stoltenberg amesema hatua hiyo ni miongoni mwa hatua za kuiunga mkono Ukraine na pia kujiwekea ulinzi binafsi wa NATO. Katibu huyo ameongezewa muda wa mwaka mmoja kuendelea kuhudumu kama katibu mkuu wa NATO. 

Wakati huo huo, kundi la viongozi wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda G7 wametangaza hatua za kuzuia matumizi ya dhahabu ya Benki Kuu ya Urusi katika shughuli za malipo, huku Marekani ikitangaza awamu mpya ya vikwazo vinavyowalenga watu binafsi, na matajiri wapatao 400 wakiwemo wanachama wa bunge la Urusi, Duma.

Kushoto: Rais wa Urusi Vladimir Putin Katikati: Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Kulia: Rais wa Marekani Joe Biden.
Kushoto: Rais wa Urusi Vladimir Putin Katikati: Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Kulia: Rais wa Marekani Joe Biden.Picha: AFP

Hapo awali, vikwazo dhidi ya matajiri wa Urusi, Benki Kuu ya nchi hiyo na Rais Vladimir Putin havikuathiri akiba ya dhahabu ya nchi hiyo, ambayo imehifadhiwa kwa miaka kadhaa.

Urusi inahodhi takriban dola bilioni 130 katika akiba ya dhahabu, na Benki ya Urusi ilitangaza mnamo Februari 28 kwamba itaanza tena ununuzi wa dhahabu kwenye soko la ndani la madini ya thamani.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Irina Yakovleva/TASS/dpa/picture alliance

Akihutubia mkutano wa kilele wa NATO wa mjini Brussels, kwa njia ya video rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema Ukraine inahitaji ndege za kivita, vifaru, silaha za kupambana na meli na ulinzi wa anga ulioboreshwa ili kuwazuia wanajeshi wa Urusi katika vita hivyo vilivyoingia katika mwezi wa pili tangu kuanza.

Baadi ya viongozi na wakuu wa nchi zenye nguvu duniani walikutana pembezoni mwa mkutano wa kilele wa NATO ambapo Rais Biden alikutana na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg huku Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron akikutana na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoganPicha: Irina Yakovleva/ITAR-TASS/imago images

Mataifa ya Magharibi yanatarajiwa kumuonya Rais Putin kwenye tamko lao la pamoja baada ya mikutano hiyo mitatu kwamba Urusi italipa gharama kubwa kutokana na kuivamia Ukraine.

Mikutano hiyo inafanyika katika mji mkuu wa kidiplomasia barani Ulaya, Brussels, Ubelgiji ambao ni mwenyeji wa mikutano hiyo ya dharura ya NATO, kundi la mataifa saba yaliyoendelea kiviwanda G7 na ule wa wanachama 27 wa nchi za Umoja wa Ulaya.

Vyanzo: AP/RTRE