1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani zaidi kati ya Ronaldo na Lewandowski?

30 Juni 2016

Robo fainali za kombe la Euro 2016 zinaanza rasmi leo(30.06.2016) na mshambuliaji wa Ureno Ronaldo anawania kupiga hatua mpya kupata taji lake la kwanza la kimataifa pale Ureno itakapokwaana na Poland mjini Marseille.

https://p.dw.com/p/1JGvs
Kombi-Bild Ronaldo Lewandowski
Cristiano Ronaldo(kushoto)wa Ureno na Robert Lewandoswki (kulia)wa Poland

Katika pambano la washambuliaji wawili hatari katika bara la Ulaya , Poland itatupa matumaini yake kwa mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski kuzima kitisho cha Cristiano Ronaldo kwa kuzifumania nyavu kwa mara ya kwanza katika michuano hii.

Island EURO 2016 Fußball Fans in Reykjavik
Mashabiki wa Iceland wakishangiria timu yaoPicha: Getty Images/AFP/H. Kolbeins

Mpambano huo unazindua siku nne za mapambano magumu ya kihistoria ambayo yatashuhudia Ujerumani ikiwania kushinda kwa mara ya kwanza katika mashindano makubwa dhidi ya Italia, Wales ikicheza kwa ajili ya kulinda hadhi ya Waingereza dhidi ya Ubelgiji na Ufaransa wenyeji wa mashindano hayo wanakabiliana na Iceland.

Poland na Ureno , zote zimepata mafanikio katika michuano ya kombe la Ulaya na kombe la dunia na zote zina nafasi ya dhahabu kuweza kujijengea jina katika kiwango cha kimataifa.

Frankreich Testspiel gegen Kamerun in Nantes
Kikosi cha UfaransaPicha: picture-alliance/AP Photo/D. Vincent

Mshindi wa pambano hilo atakumbana na ama Ubelgiji ama Wales katika nusu fainali na kuviepuka vigogo vinavyopigiwa upatu kutoroka na taji hilo.

Hakuna kujigamba

Kocha wa Ureno Fernando Santos amesema hakuna timu ambayo inaweza kujipiga kifua kuwa ni mshindi. "Hakuna timu inayoweza kusema ina uwezo zaidi, ni nusu kwa nusu."

Kurunzi itamuelekea zaidi Cristiano Ronaldo , ambaye kwa kawaida huiletea ushindi mara kwa mara Real Madrid timu anayochezea katika ngazi ya vilabu, lakini hapajapata mafanikio na timu ya kwao Ureno.

EM 2016 Fans Italien
Mashabiki wa Italia Azzuri.Picha: Getty Images/C. Villa

Lakini mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31 anapungukiwa tu na bao moja kuandika historia zaidi katika Ulaya kwa kulingana na mchezaji maarufu kutoka Ufaransa Michel Platini kwa rekodi yake ya magoli tisa katika fainali za kombe la Euro. Tayari amekuwa ni mchezaji wa kwanza kuweza kufunga mabao katika mashindano manne ya kombe hili.

Kwa upande wake Robert Lewandowski alipata mabao mengi zaidi katika michuano ya mchujo kwa ajili ya fainali hizi. Lakini hajauona mlango katika michezo minne aliyocheza katika fainali hizi nchini Ufaransa.

Wales wanaifurahia hadhi ya wasindikizaji katika mashindano haya ya Euro 2016, katika duru hii ya robo fainali dhidi ya Ubelgiji kesho Ijumaa lakini hali hiyo inaongeza ari ya uwezo wao ya kufanya makubwa.

Jerome Boateng Frankreich Evian PK
Mlinzi wa Die Mannschaft Jerome BoatengPicha: picture-alliance/dpa/A.Dedert

Die Mannschaft

Jerome Boateng na Toni Kroos wa timu ya Ujerumani , Die Mannschaft , wanasisitiza kwamba kushindwa huko siku za nyuma dhidi ya Italia hakuhesabiki kabisa wakati Die Mannschaft itakapopimana nguvu na Squadra Azzurri katika pambano lao la robo fainali siku ya Jumamosi.

Fußball Länderspiel Deutschland - Italien
Kocha wa Italia Antonio ContePicha: Reuters/M. Rehle

Kikosi cha Antonio Conte kimeonesha umahiri wake kwa kuwaweka kando mabingwa watetezi Uhispania kwa mabao 2-0 katika duru ya mtoano ya timu 16 za Euro 2016.

Kikosi cha Azzurri kilishinda kundi la E, kwa kuwagaragaza Ubelgiji kwa mabao 2-0, na kisha kuwaweka kando Uhispania siku ya Jumatatu na sasa wanakutana uso kwa macho na Ujerumani mjini Bordeaux kuwania nafasi katika nusu fainali ya Euro 2016.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Josephat Charo