Nani kuibuka kidedea Kombe la Afrika?
17 Januari 2013Kwa mwaka huu michuano ya kombe la Afrika ilipaswa kufanyika nchini Libya. Lakini haikuwezekana baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka mwaka 2011 na hali ya wasiwasi kuendelea kuwepo. Hivyo uamuzi wa kupeleka mashindano Afrika Kusini ulipitishwa. Mara ya mwisho nchi hiyo ilikuwa mwenyeji wa michuano hiyo mwaka 1996.
Max Grünewald kutoka Ujerumani ni meneja wa timu ya Ajax Cape Town, inayocheza katika daraja la kwanza la ligi ya kandanda Afrika Kusini: "Kwa Afrika Kusini ni heshima kubwa kuwa mwenyeji wa mashindano haya. Ulikuwa uamuzi wa busara kuleta michuano hapa baada ya kombe la dunia kufanyika pia hapa mwaka 2010. Viwanja vya mpira vina ubora wa hali ya juu. Miundombinu yote inayohitajika kufanikisha michuano hii inapatikana hapa."
Zambia yapewa tena nafasi kubwa ya kushinda
Mechi ya ufunguzi pamoja na fainali zitachezwa katika uwanja wa Soccer City jijini Johannesburg. Kati ya viwanja vikubwa vilivyotumika wakati wa kombe la dunia, uwanja wa Moses Mabhida ulioko Durban ndio utatumika mbali na ule wa Soccer City. Ingawa Cape Town ni mmoja kati ya miji mikubwa kabisa Afrika Kusini, hakuna mechi zitakazochezwa huko. Viwanja vilvyobakia ni vidogo zaidi na vipo katika miji ya Nelspruit, Rustenburg na Port Elizabeth.
"Hapatakuwa na shamrashamra kama wakati wa kombe la dunia. Michuano hii si maaraufu namna hiyo," anaamini Max Grünewald. Mwaka jana kombe la Afrika lilifanyika nchini Gabon na kumalizika kwa namna ambayo haikutarajiwa. Kwa mara ya kwanza, Zambia, ambayo haikuwa imepewa nafasi kubwa ya kushinda awali, ilitwaa taji kwa kuishinda timu ya Cote d'Ivoire.
Meneja Grünewald anaeleza kwamba timu hizo mbili ndizo zinazopewa nafasi kubwa ya kushinda katika michuano ya mwaka huu: "Timu ya Cote d'Ivorie na mshambuliaji nyota Drogba, iliyoshindwa kwa penalti na Zambia katika fainali za mwaka jana. Zambia kwa upande wake inapewa nafasi kubwa ya kushinda baada ya kutwaa ubingwa mwaka jana. Kisha zipo timu zinazofahamika kama Nigeria, ambazo ni za kufuatiliwa kwa makini."
Wakati wachezaji wengi nyota wa Kiafrika hivi sasa wanachezea vilabu vya soka barani Ulaya, wengine ambao bado hawajapata nafasi hiyo wanatumaini kwamba vipaji vyao vitaonekana wakati wa michuano ya kombe la Afrika.
Nafasi kwa Afrika Kusini
Nayo Afrika Kusini kama mwenyeji inataka kuudhihirishia ulimwengu tena kwamba ina uwezo wa kuandaa na kuendesha mashindano makubwa ya michezo. David Nyathi, aliyekuwa akiichezea timu ya taifa ya nchi hiyo anaeleza: "Kwetu ni nafasi ya kipekee - kwa sekta ya utalii na kwa wapenzi wa soka nchini. Tunapata hisia kwamba ulimwengu unathamini kile ambacho sisi kama nchi inayoendelea tunaweza kufanya kwa soka la kimataifa."
Katika kundi A, timu ya Afrika Kusini itakutana na Morocco, Angola na Cape Verde. Ghana, iliyofikia hatua ya robo fainali katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2010, itapamabana na timu za Mali, Niger na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Bingwa mtetezi Zambia itachuana na Nigeria, Burkina Faso na Ethiopia katika kundi C wakati kundi D likiwa na Algeria na Tunisia, pamoja na Cote d'Ivoire na Togo, zinazopewa nafasi kubwa ya kuibuka washindi.
Mwandishi: Arnulf Boettcher
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Josephat Charo