Nani atawika Cardiff? Real Madrid au Juventus?
3 Juni 2017Shirikisho la kandanda Ulaya - UEFA liliamua wiki iliyopita kuwa mpambano huo utachezwa katika uwanja huo wa Principality ambao paa lake linaweza kufungwa na kufunguliwa, kutokana na sababu za kiusalama. Mlinda mlango mkongwe wa Juve Gianluigi Buffon anasema kucheza katika uwanaj uliofunikwa paa haktakuwa na athari yoyote kwa matokeo ya mechi.
Tiketi zote zimeuzwa katika uwanja huo wenye uwezo wa kuwakaribisha watu 66,000. Mamilioni ya wengine watautazama mtanange huo kote ulimwenguni kupitia televisheni.
Real Madrid wanatafuta kuwa klabu ya kwanza kutetea kombe hilo maarufu la Ulaya kwa kulitwaa kwa mara ya 12 na kocha Zinedine Zidande anaamini kuwa uongozi wa Cristiano Ronaldo utakuwa sababu muhimu wakati timu yake ikitafuta kutimiza hilo
Ronaldo mwenye umri wa miaka 32 amekuwa katika hali nzuri msimu huu, kwa kufika idadi ya mabao 400 katika taaluma yake katika klabu ya Real wakati timu hiyo ilishinda taji la ligi kuu ya kandanda Uhispania, La Liga kwa mara ya kwanza katika miaka mitano.
Nahodha Sergio Ramos aliisaidia Real kushinda fainali ya mwaka wa 2014 wakati alifunga kwa kichwa bao la kusawazisha katika muda wa majeruhi dhidi ya mahasimu wao Atletico Madrid kabla ya kuwabwaga 4-1 katika muda wa ziada. Pia alifunga katika muda wa kawaida na mikwaju ya penalti wakati Real iliifunga Atletico katika fainali ya mwaka jana. Ramos anasema leo wanalenga kuandika historia . "lazima tuucheze kama tunawania kombe letu la kwanza. Tunataka kuhifadhi hadhi yetu kama mabingwa".
Wakati huo huo, Juventus ambayo imeshinda mataji mawili tu ya Ulaya, inacheza fainali yake ya pili katika misimu mitatu. Iliangushwa na Barcelona katika fainali ya 2015.
Kocha Massimiliano Allegri amesema Juve wanaweza kushinda Champions League ili kukamilisha mataji matatu katika msimu mmoja, baada ya kutwaa taji la ligi kuu ya kandanda Italia - Serie A na kombe la Italia.
Kipa mkongwe Gigi Buffon mwenye umri wa miaka 39, hajawahi kushinda Champions League katika taaluma yake ndefu lakini ana matumaini kuwa bahati itamwendea mara hii.
"Watu hupenda ndoto nzuri na kushinda fainali inaweza kuwa hadithi nzuri zaidi” alisema Gigi.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Sekione Kitojo