1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Schulz wapiga kura

24 Septemba 2017

Leo ni leo wajerumani kuamua kati ya Merkel na Schulz nani aiongoze nchi huku chama cha siasa kali kikiwatia khofu wajerumani wengi walojitokeza kupiga kura.

https://p.dw.com/p/2kbfS
Bundestagswahl 2017 | Stimmabgabe Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Kansela Angela Merkel amepiga kura mjini Berlin katika uchaguzi mkuu ambao kwa kiasi kikubwa huenda ukampa nafasi nyingine ya kuiongoza Ujerumani ikiwa ni muhula wake wa nne lakini ushindi wake vile vile huenda ukagubikwa na ushindi wa wazalendo wa siasa kali za mrengo wa kulia. Akiwa amevalia suruali ya rangi nyeusi na koti lake la rangi nyekundu Merkel ameonekana akitabasamu wakati akipigwa picha na waandishi habari wakati akitumbukiza kura yake katika sanduku la kupigia kura  akiwa katika kituo chake cha kupigia kura karibu na nyumbani kwake anakoishi katikati ya jiji la Berlin.

Ameandamana na  mumewe Joachim Sauer aliyekuwa ameshikilia mwamvuli uliomfunika pia Kansela huyo kumkinga mvua isimyeshee.Chama cha Kansela Merkel cha CDU sambamba na chama ndugu cha upande wa Bavaria cha CSU kwa pamoja vinashikilia idadi kubwa ya viti ambayo inaweza kuongeza kwa mujibu wa kura za utafiti wa maoni ya wananchi, dhidi ya wapinzani wake wa chama cha SDP kinachoongozwa na Martin Schulz.

Würselen Martin Schulz im Wahllokal zur Bundestagswahl
Kiongozi wa SPD Martin Schulz na mkewe Inge wakishikilia kura zaoPicha: Reuters/T. Schmuelgen

Uchunguzi wa maoni unaonesha kwamba chama kinachopinga wahamiaji na Waislamu cha AfD - Chama mbadala kwa Ujerumani huenda kikashinda kwa mara ya kwanza viti vya ubunge na hivyo kukifanya kuwa chama cha tatu chenye nguvu nchini Ujerumani katika kile ambacho kinaelezwa kwamba litakuwa ni tetemeko zito la kisiasa nchini Ujerumani.

Akishinda muhula wa nne, Kansela Merkel aliyeingia madarakani mwaka 2005 atakuwa katika nafasi sawa ya kipindi cha kutawala alichowahi kukiongoza Helmut Kohl aliyeiongoza Ujerumani kwa miaka 16 kama Kansela na mtu aliyekuwa mfano kwa Kansela Merkel binafsi. Martin Schulz  spika wa zamani wa bunge la Umoja wa Ulaya amepiga kura yake nyumbani kwao alikozaliwa magharibi ya Ujerumani katika mji wa Wuerselen ambapo amewaambia waandishi habari kwamba anaimani na matumaini makubwa ya ushindi licha ya kura za utafiti wa maoni kuonesha kwamba chama chake kinaelekea kupata kipigo kibaya.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/AFP

Mhariri:Iddi Ssessanga

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW