Nana Akufo-Addo ashinda uchaguzi Ghana
10 Desemba 2016Mwanasheria huyo wa zamani wa haki za binadamu mwenye umri wa miaka 72 alipata ushindi wa asilimia 53.8 ya kura, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.
"Sitawaangusha. Nitafanya kila kilichoko katika mamlaka yangu kuweza kutimiza matumaini yenu na matarajio," Akufo-Addo alisema mbele ya kundi kubwa la watu waliokuwa wakifurahia nyumbani kwake katika mji mkuu wa nchi hiyo Accra. "Nitafanya lililo katika uwezo wangu kulinda maslahi yenu na kuirejesha nchi yangu katika njia ya maendeleo na ufanisi."
Rais aliyeko madarakani John Mahama alikubali kushindwa jioni jana siku mbili baada ya mbio hizo za uchaguzi ambazo zilikuwa na ushindani mkubwa ambazo zilionekana kama mtihani kwa demokrasia ya nchi hiyo katika eneo ambalo limejaa madikteta na mapinduzi ya kijeshi.
Mahama alimpigia simu na kumpongeza kiongozi wa upinzani Akufo-Addo, ambaye wafuasi wa chama chake cha New Patriotic NPP walikuwa wakikusanyika kwa masaa kadhaa nje ya nyumba yake baada ya vyombo vya habari nchini humo kusema anaongoza kufuatia uchaguzi uliofanyika siku ya Jumatano.
"Ndio amekubali kushindwa," George Lawson wa chama cha New Democratic Congress NDC cha Mahama aliliambia shirika la habari la afp.
Ahadi ya kuimarisha uchumi
Akufo-Addo alifanya kampeni kwa kuahidi kuimarisha uchumi na kutengeneza nafasi za kazi.
"Rais wa Ghana ni rais wa kila raia wa Ghana," Akufo-Addo alisema, wakati fashifashi zikiruka angani na maelfu ya watu wakishangiria mitaani nje ya nyumba yake.
Waungaji mkono wa Akufo-Addo - karibu wote wakivalia nyuo nyeupe kabisa toka juu hadi chini , ikiwa ni ishara ya ushindi , walikuwa wakicheza katika uwanja wa nyumba yake kwa saa kadhaa wakitarajia hotuba yake ya ushindi.
Katika wakati fulani , walianza ghafla kuimba nyimbo ya taifa la Ghana. "Tumeshinda, " alisema Hajia Mustafa , mfanyabiasha mwenye umri wa miaka 44, akionesha tabasamu kubwa, "Nimepata rais wangu, nina chaguo langu."
Mbio hizo za uchaguzi zilizojaa hamasa kati ya Akufo-Addo na Mahama zilionekana kuwa kipimo cha uthabiti katika nchi hiyo ya Afrika yenye demokrasia imara.
Lakini hofu za ghasia kuzuka wakati wa uchaguzi hazikutokea, uchaguzi ukienda kwa amani kabisa na kufuatiwa na utulivu wakati matokeo rasmi yakiingia.
"Nafikiri Waghana wanapaswa kujisikia fahari kwa kiasi kikubwa," amesema balozi Johnnie Carson wa taasisi ya taifa ya demokrasia, chombo ambacho kilihusika na uangalizi wa uchaguzi.
"Ghana imejitofautisha katika miongo miwili na nusu kwa uaminifu na uwazi," Carson alisema. "Ni kiwango cha dhahabu cha demokrasia barani Afrika."
Nyanja za kutiliwa maanani
Hata hivyo wakati ujumbe wa uangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya ulisema kwamba Ghana "kwa kiasi kikubwa imeepuka ghasia ambazo wengi walihofia zingetokea" imezungumzia kuhusu maeneo mengine yanayotia wasi wasi.
"Matumizi mabaya ya kuwapo madarakani, ikiwa ni pamoja na kutokuwapo usawa wa kuvifikia vyombo vya habari vya dola, na gharama za kampeni ambazo hazitolewi maelezo ni maeneo ambayo Ghana inaweza kuyaangalia hapo baadaye," ulisema ujumbe huo katika taarifa.
Akufo-Addo atatumikia kipindi cha miaka minne katika nchi hiyo ambayo ilikuwa koloni la zamani la Uingereza, ambayo iliwahi kuwa nchi yenye uchumi imara ambayo imeshuhudia ukuaji wake ukizorota, thamani ya sarafu yake ikiporomoka na ughali wa maisha ukipanda.
Mahama , aliyeingia madarakani mwaka 2012 baada ya kumshinda Akufo-Addo , aliwataka wapiga kura, "kubaki katika njia kuu", akiwaahidi kuleta miradi zaidi ya miundo mbinu.
Katika juhudi zake za kuwania kiti hicho kwa mara ya tatu , Akufo-Addo alishambulia kiwango kibovu cha ukuaji wa uchumi nchini Ghana -- unaokadiriwa kukua kwa asilimia 3.3 mwaka huu wa 2016, kiwango cha chini kabisa katika muda wa miongo miwili -- na aliainisha mwelekeo wa nguvu wa kuubadilisha uchumi wa nchi hiyo.
Akufo-Addo pia aliwatahadharisha waungaji wake mkono kwamba "ni muhimu kulinda kura zao" katika juhudi za kuepuka kurudiwa kwa uchaguzi wa mwaka 2012 -- ambao Mahama alishinda kwa kura chache akipata asilimia 50.7 ya kura -- ambapo alifikisha malalamiko yake katika mahakama kuu ya nchi yake bila mafanikio.
Ghana ni mzalishaji mkubwa duniani wa zao la kakao baada ya Cote D'Ivoire na mzalishaji mkubwa wa pili wa madini ya dhahabu katika bara la Afrika baada ya Afrika kusini.
Lakini nchi hiyo ililazimika kuligeukia shirika la fedha la kimataifa IMF mwaka 2015 kwa hatua za uokozi wakati bei za dunia za bidhaa zilipoanguka.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusra Buawayhid