NAIROBI: Wanajeshi wa Ethiopia wakishambulia kituo cha Kenya kimakosa
3 Januari 2007Wanajeshi wa Ethiopia wakitumia helikopta za kivita walikilipua kimakosa kituo kimoja katika mpaka wa Kenya jana jioni. Maofisa wa usalama nchini Kenya wamesema ndege za kivita zilitumwa haraka katika eneo hilo.
Afisa wa ngazi ya juu wa polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema helikopta nne za Ethiopia ziliulenga mji wa Somalia wa Dhobley, yapata kilomita tatu kutoka mpakani lakini badala yake zikaangusha mabomu matatu katika kituo cha mpakani cha Har Har upande wa Kenya.
Aidha afisa huyo alisema helikopta hizo zilirudi tena na kuangusha mabomu mengine matatu. Hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu majeruhi na uharibifu uliosababishwa na mabomu hayo.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya rais Mwai Kibaki wa Kenya kukutana na kamati ya usalama ya kitaifa katika ikulu yake mjini Mombasa.