1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI : Waasi wa LRA wataka mazungumzo yawe Kenya

13 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCbE

Wawakilishi wa kundi la waasi wa Uganda la LRA wanataka mazungumzo ya amani na serikali yafanyike nchini Kenya badala ya kusini mwa Sudan ambako wamesema hawatakiwi.

Mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa kwa mzozo huo wa Uganda Rais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano anatazamiwa kuhudhuria kuanza tena kwa mazungumzo hayo katika mji mkuu wa kusini mwa Sudan wa Juba hapo Jumatatu kwa nia ya kukomesha vita vilivyodumu kwa muda mrefu kabisa barani Afrika.

Lakini Martin Ojul kiongozi wa timu ya amani ya waasi wa LRA amesema wajumbe wake wameondoka kutoka Juba kutokana na kuharibika kwa uhusiano na Sudan.

Taarifa hiyo ya LRA inakuja siku tatu baada ya Rais Sudan Omar Hassan la Bashir kuapa kwamba atawatokomeza waasi wa LRA kutoka Sudan.

Serikali ya Uganda imekataa kubadili mahala pa mazungumzo hayo ya amani kutoka Juba.