1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nairobi. Umoja wa Ulaya wataka uchunguzi ufanywe kuhusiana na uendeaji kinyume haki za binadamu Somalia.

16 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CI1f

Wabunge wa umoja wa Ulaya wametoa wito jana wa kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi kuhusiana na uhalifu wa kivita na uendeaji kinyume haki za binadamu katika mji mkuu wa Somalia, ambako serikali inapambana na waasi.

Katika taarifa wabunge hao wamesema jana kuwa azimio lililopitishwa na bunge la umoja wa Ulaya , linashutumu vikali hali ya uendeaji kinyume haki za binadamu zinazofanywa na pande zote katika mzozo huo.

Azimio hilo pia linatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na hususan kuachwa mara moja kwa mashambulizi dhidi ya raia. Mwezi wa Aprili, mwaka huu mjumbe wa umoja wa Ulaya nchini Kenya , Eric van der Linden ameutaka uongozi wa umoja wa Ulaya kuchunguza iwapo majeshi ya Ethiopia na ya Somalia yamekuwa yakifanya vitendo vya uhalifu wa kivita katika msako wao dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu na wa kiukoo mjini Mogadishu. Rais wa Somalia Abdullahi Yusuf Ahmed , akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi , amethibitisha kutokea kwa maafa hayo, akisema kuwa wapiganapo tembo ziumiazo ni nyasi.