Nairobi. Tume ya haki za binadamu nchini Kenya yaitaka serikali ya nchi hiyo kutoyumbishwa na Marekani kutaka itie saini makubaliano kwamba raia wa Marekani wasishtakiwe katika mahakama ya kimataifa.
4 Juni 2005Serikali ya Kenya imezidi kupata shinikizo jana Ijumaa kukataa kutia saini makubaliano na serikali ya Marekani yanayotoa uwezo wa raia wa Marekani kutoshitakiwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC.
Muda mfupi baada ya serikali kudai kuwa kuna njama za kubanwa na serikali ya Marekani kuhusu suala hilo, makundi ya haki za binadamu nchini humo na wabunge wameitaka serikali kukataa wito wa Marekani wa kutiwa saini kwa makubaliano hayo.
Tume ya taifa ya haki za binadamu nchini Kenya, KNCHR, ambayo ni kamati ya kuishauri serikali, imesema kuwa vitisho vya Marekani vya kuacha kuipatia Kenya dola milioni 20 za msaada muhimu wa kijeshi iwapo makubaliano hayo hayatafikiwa ni kuiburuza Kenya na kuiweka rehani kwa ajili ya fedha.
Kamishna wa tume hiyo Bibi Catherine Mumo ameishutumu Marekani kwa kutumia mbinu za kikoloni na kudai kile itakacho kwa nchi hiyo ya Afrika mashariki.