Waarmenia wa Karabakh wakubali kusitisha mapigano
20 Septemba 2023Vikosi vya jamii ya Waarmenia wanaotaka kujitenga kwa jimbo la Nagorno-Karabakh vimesema vimekubaliana na masharti ya kusitisha mapigano yaliyopendekezwa na walinda amani wa Urusi.
Tangazo hilo la kukubali usitishaji wa mapigano limetolewa na Waarmenia wa Nagorno Karabakh, chini ya uongozi wa wanachokiita Jamhuri ya Artsakh waliyoitangaza wenyewe.
Hayo yamejiri baada ya kundi hilo lenye silaha kukumbwa na msururu wa vipigo kutoka kwa jeshi la Azerbaijan.
Soma pia: Marekani na Urusi zatoa mwito wa utulivu jimboni Nagorno Karabakh
Katika tangazo lao wamesema vikosi vya Azerbaijan vimefanikiwa kuvunja ngome zao za ulinzi na kukamata maeneo kadhaa ya kimkakati, na kuongeza kuwa katika mazingira kama hayo hawana chaguo jingine zaidi ya kusimamisha mapigano ifikapo saa saba mchana majira ya eneo lao.
Wizara ya Ulinzi ya Azerbaijan imethibitisha makubaliano ya kusitisha mapigano, ikisema waasi wa Armenia waliojitenga wamekubali "kuweka chini silaha zao, kuacha maeneo ya mapigano na vituo vya kijeshi na kusalimisha kikamilifu silaha," huku silaha zote na vifaa vizito vikikabidhiwa kwa jeshi la Azerbaijan.
Makubaliano hayo yalitarajiwa kuanza kutekelezwa saa moja jioni kwa saa za eneo hilo na mazungumzo ya amani kati ya maafisa wa Azerbaijan na wanaotaka kujitenga sasa yamepangwa kufanyika siku ya Alhamisi katika mji wa Yevlakh wa Azerbaijan.
Nagorno Karabakh inatambuliwa kimataifa kama eneo la Azerbaijan.
Urusi yahamisha zaidi ya raia 2,000 Nagorno-Karabakh
Wanajeshi wa kulinda amani wa Urusi walisema wamewahamisha zaidi ya raia 2,000 wakiwemo zaidi ya watoto 1,000 kutoka maeneo "hatari zaidi" huko Nagorno-Karabakh, siku moja baada ya Azerbaijan kuanzisha operesheni yake ya kijeshi.
Soma pia: Maelfu ya watu waandamana Karabakh wakitaka kufunguliwa barabara inayounganisha Armenia
"Kikosi cha kulinda amani cha Urusi kinaendelea kuwahamisha raia wa Nagorno-Karabakh kutoka maeneo hatari zaidi," Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema katika taarifa.
Hapo awali, Wizara ya Mambo ya Nje ya Armenia ilitoa wito kwa walinda amani wa Urusi walioko Nagorno-Karabakh "kuchukua hatua za wazi na zisizo na shaka kukomesha" mapigano.
Papa anazitaka pande zote 'kunyamazisha silaha zao'
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis aliunga mkono juhudi za amani kwa ajili ya watu wa Nagorno Karabakh kwa kuzitaka pande zote "kunyamazisha silaha zao".
"Kwa mara nyingine nazitolea mwito pande zinazohusika, na jumuiya ya kimataifa kunyamazisha silaha, na kufanya kila juhudi kutafuta suluhisho la amani kwa ajali ya watu na heshima kwa ubinadamu,'' alisema kiongozi huyo wa Kanisa.
Tangu Azerbaijan ianzishe operesheni yake ya kijeshi Nagorno-Karabakh siku ya Jumanne, Marekani, Urusi, EU na Umoja wa Mataifa zimetoa wito kwa pande zinazozozana kukomesha mara moja uhasama.
Mazoezi ya pamoja ya Marekani na Armenia kumalizika kama ilivyopangwa
Wanajeshi wa Marekani watakamilisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi na vikosi vya Armenia nchini Armenia siku ya Jumatano kama ilivyopangwa, na hayakuathiriwa na operesheni kubwa ya kijeshi ya Azerbaijan, msemaji wa jeshi la Marekani alisema.
Soma pia: Armenia, Azerbaijan zaelekea kupata suluhu ya Nagorno-Karabakh
Msemaji huyo alisema hakujawa na mabadiliko yoyote katika zoezi la siku 10 la Eagle Partner 2023 lililohusisha wanajeshi 85 wa Marekani na Waarmenia 175, licha ya Azerbaijan kuanzisha operesheni iliyoiita "ya kupambana na ugaidi" katika eneo la Nagorno-Karabakh siku ya Jumanne.
"Tulifahamu kwamba walikuwa wanaendesha operesheni lakini hatukutathmini kuwa kuna hatari yoyote kwa askari wetu wakati huo na hivyo walibaki kwa muda wote wa zoezi hilo," alisema msemaji huyo.
Baada ya miezi kadhaa ya kuongezeka kwa mvutano katika eneo la Nagorno-Karabakh linalodhibitiwa na Armenia kusini mwa Caucasus, Azerbaijan siku ya Jumanne ilituma wanajeshi wakiungwa mkono na mashambulio ya mizinga katika eneo hilo katika jaribio la kulilaazimisha eneo hilo kusalimu amri.
Eneo hilo la milima ya Nagorno-Karabakh inatambulika kimataifa kama sehemu ya Azerbaijan, lakini sehemu yake inaendeshwa na mamlaka za Kiarmenia zinazotaka kujitenga ambazo zinadai kuwa ni nchi ya mababu zao.
Chanzo: Mashirika