1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bankenfusion Deutschland

Charo, Josephat1 Septemba 2008

Je kuungana kwa benki ya Commerzbank na Dresdner kutainufaisha Ujerumani huku nafasi za ajira 9000 zikikaribia kupunguzwa?

https://p.dw.com/p/F8rO
Makao makuu ya benki ya Commerzbank (kushoto) na benki ya Dresdner yaliyozinduliwa mjini FrankfurtPicha: AP

Kwa takriban euro bilioni kumi benki ya Commerzbank imeinunua benki ya Dresdner. Hii ina maana benki ya tatu kwa ukubwa hapa Ujerumani imeinunua benki iliyo ya pili kwa ukubwa. Hatua hiyo inasababisha kuchipuka kwa benki mpya yenye mali ya thamani ya euro bilioni 1,100 lakini benki ya Deutsche Bank bado inashikilia nafasi ya kwanza ikiwa na mali yenye thamani karibu mara mbili ya hiyo.

Tayari waziri wa fedha wa Ujerumani Peer Steinbruck ameisifu hatua ya benki ya Commerzbank kuinunua benki ya Dresdner akisema itaimarisha sekta ya benki ya Ujerumani. Hii ni kwa sababu kumechipuka sasa benki mpya kubwa ya Ujerumani itakayokuwa na ushawishi mkubwa katika soko la hisa. Benki hizo zinaleta pamoja na mali ya thamani ya euro bilioni 1,100, kiwango ambacho kwa kweli ni nusu tu ya mali ya beni ya Deutsche Bank ambayo inashikilia nafasfi ya kwanza kwal ukubwa hapa nchini.

Kwamba muungano wa benki ya Commerzbank na Dresdner ni wa pili kwa ukubwa haitoshi kitu, cha muhimu ni uwezo wake wa kifedha. Sababu kwa nini benki kubwa ya Dresdner imenunuliwa na benki ndogo ya Commerzbank kwa kwamba benki hiyo imekuwa dhaifu.

Benki ya Commerzbank iliacha kufanya biashara ya kimataifa katika miaka michache iliyopita na kujishughulisha zaidi na kuwapa mikopo wafanyabiashara wa tabaka la katikati hapa Ujerumani. Hiyo bila shaka ndiyo sababu kwa nini benki hiyo haijaathiriwa sana na mzozo wa kimataifa wa mabenki.

Benki ya Commerzbank ni ndogo lakini inaongozwa vizuri na inazisimamia vyema biashara zake. Ndio maana hata wakati mgumu inapata faida.

Hali lakini ni tofauti kabisa katika benki ya Dresdner. Imejaribu kila kitu lakini imefaulu kwa asilimia ndogo sana. Hatua yake ya kutoa mikopo ya nyumba mfano wa mabenki ya Marekani imesababisha mabilioni ya euro kupotea.

Benki hiyo inakabaliwa na tatizo kubwa la kifedha karibu kuwa muflisi. Kampuni ya bima ya Allianz inayoimiliki benki ya Dresdner ilijaribu kuisaidia benki hiyo lakini pasipo mafanikio.

Kampuni hiyo haukuthamini sana biashara ya benki bali biashara ya bima ndio maana ikawekeza zaidi katika matawi yake ya bima badala ya kutoa fedha zaidi kuiokoa benki ya Dresdner. Pesa nyingi zilipotea, lakini hata hivyo mwaka wa 2001 kampuni ya Allianz ikainunua benki hiyo kwa kiasi cha euro takriban bilioni 24.

Baada ya muda mrefu na kwa misingi ya msimamo usemao afadhali mwisho wenye matatizo kuliko matatizo yasiyo na mwisho, kampuni ya Allianz inaachia uongozi wa benki ya Dresdner lakini itabakia kumiliki asilimia 30 ya hisa kwenye muungano wa benki hiyo na benki ya Commerzbank.

Hatua hiyo ina faida kwa kampuni ya bima ya Allianz kwamba itaweza kuachana na baadhi ya huduma zake za bima na iitumie benki hiyo kwa kuwa imeungana na benki kubwa ya pesa.

Ubaya wake kama kawaida ni kupunguzwa kwa nafasi 9,000 za ajira nyingi kati yao zikiwa hapa Ujerumani. Katika makao makuu ya benki mpya mjini Frankfurt nafasi za ajira zinafanana. Ndio maana baadhi ya nafasi hizo katika benki mpya ya muungano hazitahitajika tena. Pia thuluthi moja ya matawi 2000 ya benki za Commerzbank na Dresdner yatafungwa kutokana na hatua yao ya kuungana.

Kuungana kwa benki ya Commerzbank na Dresdner kumeinyima nafasi benki ya maendeleo ya China iliyotaka pia kuinuna benki ya Dresdner na kuandeleza masilahi ya kibiashara ya China hapa nchini. Lakini haikuweza kubainika wazi serikali ya China ingefanya nini na benki hiyo ya Dresdner.

Sasa kutakuwa na mashindano makali kutokana na kuchipuka kwa benki hii mpya, lakini haitakuwa changamoto kubwa kwa benki ya Deutsche Bank inayofanya biashara ya kimataifa. Hata hivyo katika masoko ya hisa ya Ujerumani benki ya Commezbank itakuwa na jukumu kubwa.