Mzozo wa nyuklia baina ya Iran na Umoja wa Ulaya na Abdu Mtullya
8 Agosti 2005Katika pendekezo hilo nchi za Umoja wa Ulaya zikiungwa mkono na Marekani zimesema zipo tayari kuiruhusu Iran iendeleze mradi wake wa nyuklia kwa madhumuni ya amani ikiwa nchi hiyo itaacha mpango wa kurutubisha madini ya uranium.
Iran imekataa pendekezo hilo, na kamati ya masuala ya mambo ya nje ya bunge la nchi hiyo inataka mpango wa kurutubisha madini ya Uranium uanze tena katika mtambo wa Isfahan.
Nchi za Ulaya ,hasa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa zimekuwa zinajaribu kufikia usikizano na Iran juu ya kutatua mzozo huo wa nyuklia.
Hatahivyo wadadisi wa masuala ya kimataifa wanasema kwamba pendekezo la nchi za Ulaya kimsingi halina jambo jipya.
Iran kwa upande wake imesema kwamba pendekezo hilo linainyima nchi hiyo haki ya kurutubisha madini ya uranium.
Iran imesisitiza haki hiyo kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa uliotiwa saini na nchi hiyo; kwamba nchi hiyo kama nyingine zilizotia saini mkataba huo pia ina haki ya kutengeneza nyenzo zote zinazohitajika kwa ajili ya mpango wake wa nyuklia.
Uamuzi wa Iran kukataa pendekezo la nchi za Ulaya unajenga mawezekano makubwa juu ya nchi hiyo kufikishwa mbele ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Shirika la nishati ya nyuklia duniani IAEA kesho linatarajiwa kufanya kikao cha dharura kutafakari suala hilo.
Hatahivyo Iran imesema haina wasi wasi wowote juu ya kufikishwa mbele ya Umoja wa Mataifa kama msemaji wa wizara ya mambo ya nje bwana Assefi alivyoeleza.
Iran imesema uamuzi wa kuifikisha nchi hiyo kwenye Umoja wa Mataifa utakuwa umechukuliwa kwa sababu za kisiasa.
Wakati huo huo wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wamewasili nchini Iran ili kuweka vifaa vya kufuatilia shughuli zinazofanyika katika mtambo wa Isfahan baada ya Iran kusema kwamba sasa inadhamiria kuanza tena shughuli za kurutubisha madini ya Uranium. Wakaguzi hao wataweka kamera maalumu zitakazoonyesha iwapo Iran imevunja vizuizi vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa.
Hapa nchini Ujerumani Kansela Gerhard Schröder ameeleza wasi wasi juu ya uamuzi wa Iran.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa bwana Philippe Douste-Blazy ameitaka Iran ijaribu kusikiliza mashauri ya busara.
Lakini Iran imesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba haitanza tena shughuli zake za kinyuklia katika sekta nyeti.
.