1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa fedha na uchumi ukabiliwe pamoja

19 Machi 2009

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kabla ya kwenda Brussels kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya, alihutubia Bunge la Ujerumani mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/HFnZ
Bundeskanzlerin Angela Merkel gestikuliert am Donnerstag, 19. Maerz 2009, waehrend ihrer Rede im Bundestag in Berlin. (AP Photo/Michael Sohn) --- German Chancellor Angela Merkel is seen during her speech at the German Federal Parliament in Berlin, Germany, Thursday, March 19, 2009. (AP Photo/Michael Sohn)
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akihutubia Bunge la Ujerumani Bundestag mjini Berlin.Picha: AP

Katika hotuba hiyo, Merkel alitoa mwito wa kushirikiana na kuukabili mgogoro wa fedha na uchumi unaodorora. Kansela Merkel amesema ushirikiano ni njia bora kabisa ya kupambana na mgogoro wa uchumi na kurejesha imani katika masoko ya fedha. Lengo mojawapo la mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya ni kuwa na msimamo mmoja kuhusu sheria za kudhibiti masoko ya fedha kabla ya mkutano wa kundi la nchi 20 zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi-G20-utakaofanywa mwanzoni mwa mwezi wa Aprili mjini London.

Kansela Merkel amezionya serikali kutoanzisha mipango mipya ya dharura kufufua uchumi kabla ya kuona iwapo hatua zilizochukuliwa zinaonyesha ishara za kufanikiwa. Ujerumani iliyotoa Euro bilioni 400 katika mradi wa Umoja wa Ulaya kusaidia kunyanyua uchumi, ni miongoni mwa nchi zilizotoa msaada mkubwa kabisa. Ujerumani, ikiongoza duniani kwa mauzo yake ina hamu kubwa ya kuhakikisha kuwa uchumi unaimarika kote duniani. Kwa maoni ya Kansela wa Ujerumani, Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ingweza kusaidia zaidi kwa kuchukua hatua za mpito za kuregeza masharti ya ruzuku, kuharakisha utataratibu wa kupitisha maamuzi na kurekebisha maafikiano yanayohusika na utulivu na ukuaji wa kiuchumi-maafikiano ambayo husimamia matumizi ya serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Bibi Merkel ameeleza kuwa mazungumzo yamefanywa kati ya Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF na Benki ya Maendeleo ya Ulaya kusaidia kupanga upya mifumo ya fedha katika Ulaya ya Kati na Mashariki-maeneo yaliyoathirika sana kutokana na mgogoro wa uchumi. Wakati huo huo, Angela Merkel amesema kila mwanachama au hata wanaohitaji kusaidiwa wanapaswa kuwajibika kwa sehemu kubwa. Kuna masuala mawili ya kujiuliza:

"Kwanza, ni vipi hatua za kitaifa za kupambana na mgogoro wa uchumi na fedha zichukuliwe bila ya kuwa kipingamizi na kusababisha mapambano ya maslahi kati ya wanachama.Pili hatua gani ziichukuliwe ili mgogoro wa aina hii usitokee tena katika siku zijazo."

Merkel anaepinga kutoa fedha zaidi kabla ya kuona matokeo ya hatua zilizochukuliwa hadi hivi sasa,amesema ni matumaini yake kuwa mkutano ujao wa G20 utaweza kukubaliana hatua zitakazohakikisha kuwa matumizi ya serikali daima hayotopindukia pato lake.Kinachohitajiwa ni mipango ya kufufua uchumi na sio kushindana kwa kile kisichoweza kutekelezwa.

Mwandishi: P.Martin/DPAE/ZPR

Mhariri: O.Miraji