1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa fedha magazetini

Hamidou, Oumilkher13 Oktoba 2008

Mpango wa serikali kuu ya Ujerumani wa kutenga yuro bilioni 400 kuzinusuru benki zisifilisike

https://p.dw.com/p/FYRS
Waziri wa fedha akiwasilisha mpango wa serikali kuu bungeni mjini BerlinPicha: AP



Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo wameuchambua zaidi mpango wa kuunusuru mfumo wa fedha wa kimataifa.Mada nyengine magazetini ni pamoja na kushindwa mwenyekiti mteule wa walinzi wa mazingira "Die Grüne" Cem Özdemir katika juhudi zake za kutaka akubaliwe kutetea kiti cha bunge la shirikisho-Bundestag.

Tuanze lakini na mpango wa serikali kuu ya Ujerumani wa kutenga mabilioni ya Yuro kwaajili ya kuzinusuru benki zisifilisike.Gazeti la DIE WELT linaandika.



Litakua balaa kubwa ikiwa mpango huo wa serikali kuu utapingwa na wabunge kama ilivyoshuhudiwa wakati serikali ya Marekani ilipowasilisha mpango kama huo katika baraza la Senet.Wabunge wa siasa kali za mrengo wa kushoto hawataicha fursa ya kuutia ila mpango huo kwa kusema utagharimiwa kwa fedha za kutoka fuko la huduma za jamii.Wengine watahoji mpango huo  utapelekea kutaifishwa mashirika. Wababe wa vyama vinavyounda  serikali kuu ya muungano watalazimika kujitokeza na hoja kali zaidi kuweza kuzishinda nguvu hoja hizo mbili.



Hayo ni maoni ya Die Welt.Gazeti la Die TAGESZEITUNG linahisi mipango ya serikali kuu haitoshi.Gazeti linaendelea kuandika:


"Serikali inajipatia ushawishi kwa kudhamini misaada,-hayo ni kwa mujibu wa waziri wa fedha Steinbrück.Sasa kwanini wasishauri hisa sawa kulingana na fedha taslim?Kwa kuchangia visenti tuu,serikali ingeweza moja kwa moja kuwa na haki ya kupitisha maamuzi  na kwa ushirikiano pamoja na wawakilishi wa waajiriwa,kufika hadi ya kua na wingi wa kura katika baraza la usimamizi.Kwa namna hiyo kila kitu kingerekebishwa-jambo ambalo ni la maana.Kwanini basi wanasita sita?


Kuingilia kati serikali katika sekta ya fedha ni upuuzi mtupu,linahisi gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE na kuendelea:


"Ni pigo kwa mfumo bora wa maisha, uchumi wa kijamii na uchumi wa soko huru.Yaonyesha hakuna njia nyengine,lakini kwa mtazamo wa muda mrefu mtu hatokosa kugundua kwamba serikali si shirika nzuri.Itabidi siku moja irejee nyuma na hayo hata kansela mwenyewe anayajua.Lakini hadi wakati huo utakapowadia,wale watakaotumia misaada watakua wameshatambua serikali  inawadhibiti.Benki haziwezi kutegemea kugharimia shughuli zao kwa msaada wa walipa kodi.


Mada ya pili magazetini ni kuhusu kushindwa mwanasiasa wa chama cha walinzi wa mazingira Die Grüne Cem Özdemir kuteuliwa katika mkutano mkuu wa chama chake huko Baden-Württemberg,kutetea kiti cha bunge,uchaguzi mkuu utakapaoitishwa mwakani.Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linaaandika.


"Kosa,ambalo mtu hakutarajia kama lingetokea chamani.Katika mkoa wa Schwäbisch huko Gmünd,wafuasi wa chama hicho wametaka kuzuwia  kile ambacho ni kawaida katika daraja ya shirikisho:Yaani kutenganisha wadhifa wa uongozi wa chama na kukalia kiti cha bunge.Mwenye kuongoza chama,haruhusiwi kuketi bungeni wanasema.Cem Özdemir angekua msaada mkubwa kwa mwenyekiti mwenza Claudia Roth.Lakini yadhihirika kana kwamba walinzi wa mazingira die Grüne huko Baden-Württemberg hawajali wakubwa wao mjini Berlin wanataka nini.