Mzozo wa Euro unahatarisha uchumi duniani
20 Septemba 2011Wakati huo huo, Ugiriki inayokabiliwa na kitisho cha kufilisika, inajitahidi kama iwezavyo, kupata msaada wa dharura kutoka kwa Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF. Waziri wa Fedha wa Ugiriki, Evangelos Venizelos ameashiria kuwa serikali yake ipo tayari kuchukua hatua kali zaidi za kubana matumizi na kupunguza nakisi katika bajeti. Mkutano uliofanywa kwa njia ya simu, jana usiku, kati ya waziri huyo wa fedha na wataalamu wa kiuchumi wa Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, ulimalizika haraka bila ya mafanikio makubwa kupatikana.Hata hivyo, Venizelos amesema, majadiliano hayo yalikuwa na manufaa na umuhimu. Kwa mujibu wa wizara ya fedha ya Ugiriki na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, majadiliano hayo yataendelea leo jioni kwa njia ya simu.
Hapo awali, mwakilishi wa IMF nchini Ugiriki, Bob Traa alifafanua hatua zinazopaswa kuchukuliwa na serikali ya Ugiriki ili kuweza kupata mkopo wa Euro bilioni 8 unaohitajiwa kwa dharura na nchi hiyo. Alieleza:
"Kwa maoni yetu, kodi ya pato isiendelee kupandishwa. Kwani hiyo ni hatua isiyoweza kuendelezwa kiuchumi wala kisiasa."
Anasema, kwanza serikali ya Ugiriki inapaswa kurekebisha mfumo wa kutoza kodi, kwani mpaka sasa haukuleta matokeo yaliyotazamiwa. Vile vile ichukue hatua kali kupambana na tatizo kubwa la wakwepa kodi.Ripoti nzuri kutoka kwa wataalamu hao ndio itakayosaidia kuamua, iwapo Ugiriki ipewe kitita hicho cha Euro bilioni 8 kutoka msaada wa fedha wa Euro bilioni 110 uliokubaliwa hapo awali. Taarifa rasmi kutoka Athens zinasema, ikiwa Ugiriki haitopewa fungu hilo la fedha, basi serikali inakabiliwa na kitisho cha kufilisika mwezi wa Oktoba.
Kwa upande mwingine, Italia nayo leo imepata pigo, baada ya shirika la Standard & Poor´s kushusha kiwango cha uwezo wa nchi hiyo kulipa madeni yake. Hatua hiyo imeshtusha na imesababisha thamani ya Euro kuanguka katika masoko ya fedha asubuhi ya leo. Vile vile inazidisha wasiwasi katika kanda inayotumia sarafu ya Euro. Wachambuzi wanasema, hatua hiyo itaathiri uchumi duniani kwa hivyo viongozi hawana budi kuwa na msimamo mmoja na kuchukua hatua imara kuutenzua mzozo wa madeni katika kanda ya Euro. Kwa maoni ya wataalamu wa kiuchumi, mzozo huo wa fedha unapaswa pia kushughulikiwa kwa dharura katika mikutano ya IMF, Benki ya Dunia na kundi la G20 linalojumuisha nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi duniani, inayofanywa wiki hii mjini Washington, Marekani.
Mwandishi:Martin,Prema
Mhariri: Josephat Charo