Mzee Kaunda apendekeza serikali ya umoja wa kitaifa Zimbabwe
8 Juni 2008Matangazo
Kenneth Kaunda rafiki wa karibu wa Mugabe amesema kuna haja ya kufikiria upya juu ya marudio ya uchaguzi wa rais kati ya hao wawili yaliopangwa kufanyika hapo tarehe 27 mwezi wa Juni kwa kusema kwamba hayatoleta amani katika nchi hiyo iliokumbwa na mzozo wa kisiasa na kiuchumi kwa miaka kadhaa.
Kaunda amesema katika taarifa kwamba hali ya Zimbabwe haiwezi kusaidiwa na aina yoyote ile ya matokeo ya uchaguzi wa rais wa Juni 27.
Amependekeza kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa sawa na ile ilioundwa nchini Kenya mwaka huu kukomesha umwagaji damu kufuatia uchaguzi uliozusha utata.
Rais huyo wa zamani wa Zambia alietawala kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1991 amesema madaraka kati ya rais na waziri mkuu lazima yagawiwe sawa sawa.