Myanmar yahusishwa na mauwaji
22 Aprili 2013Shirika hilo limetoa tuhuma hizo kwa kuzingatia ushahidi wa makabuli ya halaki na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu waliopoteza makaazi yao.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo lenye makao yake New York nchini Marekani, kabila la Rohingya, ambao wanadai kuwa ni raia wa taifa hilo ambalo vilevile linajulikana kama Burma, wanakabiliwa na vitendo vya kihalifu dhidi ya binaadamu yakiwemo mauwaji, mateso,kufukuzwa na kulazimika kuhama makazi yao.
Makundi ya wahusika wa tuhuma
Human Rights Watch limewataja maafisa wa Myanmar, viongozi kwa umma na viongozi wa madhehebu ya Budha kwamba wanapanga na kuvishawishi vikundi mbalimbali ambavyo vinaungwa mkono na vikosi vya usalama kufanya mashambulio ya kupanga katika vijiji vya waislamu mwezi Oktoba, huko katika jimbo la magharibi la Rakhine nchini humo.
Phil Robertson ambae ni naibu mkurugenzi wa shirika hilo katika kanda ya Asia alisisitiza kufanywa kwa vitendo hivyo kwa kudai serikali ya Myanmar inajihusisha vitendo hivyo vya ukandamizaji ambavyo vinaendelea mpaka sasa kwa kushindwa kulitambua kundi hilo la watu na kuwazuwia wasitembee kutoka sehemu moja kwena nyingine.
Hatma ya vikwazo wa Myanmar
Ripoti hii ya Human Right Watch inatolewa siku moja sambamba na siku ambayo Umoja wa Ulaya unatarajiwa kuondowa vikwazo vyake vyote vilivyosalia isipokuwa vya silaha. Kutokana na hayo Robertson anasema ni hatua ya mapema na iliyokosa maana na kwamba itashusha hadhi ya uhusiano wa Umoja Ulaya na utawala wa nchi hiyo
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bangkok, kiongozi huyo wa Human Rights Watch ametoa wito kwa nchi wahisani zikiwemo Marekani kushinikiza Myanmar kuhamasisha mabadiliko ya kidemokrasia katika taifa hilo ambalo lilifikisha kikomo miongo kadhaa ya utawala wa kijeshi mwaka 2011.
Akielezea hali ilivyo katika jimbo la Rakhine, Robertson alionya kama hali itaendelea kama ilivyo sasa katika eneo hilo basi uenda ikazorotesha mchakato wa mabadiliko ya kidemokrasia nchini humo.
Serikali yapuuza ripoti ya HRW
Lakini msemaji wa rais wa Myanmar alilituhuma shirika la hilo kwa kutoa hadharaini ripoti yao wakati huu ambapo Umoja wa Ulaya ukitarajiwa kutoa uamuzi kuhusu vikwazo ilivyowekewa taifa hilo. Katika maelezo yake aliyoyachapisha katika ukurasa wa face book afisa huyo wa Ikulu amesema serikali itaipuuzilia mbali ripoti hiyo ya upande mmoja.
Alisema serikali inasuburi matokeo ya ripoti ya kamisheni ya timu ya maafisa wake ambao wanafanya uchunguzi ambayo hata hivyo ripoti hiyo imekuwa ikiahirishwa mara kadhaa kutolewa.
Ripoti hii ya Human Rights Watch inasema zaidi ya watu 125,000 wa Kabila la Rohingya na makundi mengine ya kiislamu wamelazimishwa kubaki pasipo makazi na kwamba wanakosa misaada ya kiutu na pia kushindwa kurejea katika makazi yao. Takwimu za serikali zinasema takribani watu 211 waliwawa katika awamu mbili tofauti za mapigano 2012 ingawa wachambuzi wanasema idadi inaweza kuwa kubwa zaidi
Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman