Mwili wa mhanga wa ubakaji wachomwa
30 Desemba 2012Tukio hilo lilifanyika saa kadhaa baada ya mwili wa marehemu kurejeshwa nchini humo kutoka Singapore.
Mwanamke huyo ambaye hakutajwa jina lake mwenye umri wa miaka 23, ambaye alisababisha maandamano makubwa nchi nzima tangu aliposhambuliwa kinyama katika basi mjini New Delhi wiki mbili zilizopita, alichomwa moto bila kuwapo watu ambao wangeshuhudia tukio hilo kwa ombi la wazazi wake waliokuwa na fadhaa kubwa.
Taratibu za mazishi
Taratibu hizo za mazishi za kuchoma moto , zilifanyika baada ya ndugu na marafiki kufanya taratibu za mwisho za maombi kwa muda mfupi katika wilaya ya kusini magharibi ya Dwarka mjini Delhi, kwa mujibu wa waombolezaji ambao wamemweleza msichana huyo ambaye alikuwa mwanafunzi wa taaluma ya udaktari kuwa alikuwa mtu anayetambulika na wengi na mwenye kipaji.
"Nimekuja kwa sababu nilikuwa nampenda kwa dhati msichana huyu. Alikuwa mtu mwenye uwezo mkubwa kuliko wasichana wengine wote katika eneo tunakoishi," amesema Meena Rai, ambaye alikuwa rafiki wa karibu na jirani.
Waziri mkuu awataka Wahindi kuwa watulivu
Waziri mkuu Manmohan Singh na Sonia Gandhi, kiongozi wa chama kikuu tawala cha Congress, walikuwa katika uwanja wa ndege mjini New Delhi kuwapa pole wazazi wa msichana huyo wakati mwili wake ulipokuwa ukiwasili nyumbani kwa ndege ya kukodi ikiwa na mwili wa mtoto wao.
Baada ya matibabu ya awali katika hospitali mjini Delhi , alipelekwa nchini Singapore siku ya Jumatano usiku. Lakini madaktari wameshindwa kuzuwia viungo vyake kadha vilivyoshindwa kufanyakazi na alitangazwa kuwa amefariki katika saa za alfajiri siku ya Jumamosi(29.12.2012).
Kifo chake kilisababisha serikali kuahidi ulinzi bora zaidi kwa wanawake, na tathmini ya kina kwa taifa hilo ambapo matukio ya ubakaji hutokea kila siku na udhalilishaji huo wa kingono hupuuziwa kila mara, kama mchezo wa mzaha tu.
Wimbi la maandamano lilizuka nchini India tangu shambulio hilo usiku wa Desemba16 wakati mwanamke huyo alipofanyiwa unyama huo pamoja na kushambuliwa kwa kupigwa kwa chuma, na kusababisha kupata majeraha mabaya tumboni.
Mishumaa yawashwa kumuenzi marehemu
Maelfu ya watu walishiriki katika tukio la kuwasha mishumaa usiku siku ya jumamosi (29.12.2012) baada ya waziri mkuu Singh kuongoza miito ya kuwataka watu kuwa watulivu na kuepusha kurejewa kwa maandamano yaliyokuwa na ghasia.
Msichana huyo alitarajia kuolewa na mpenzi wake ambaye nae alijeruhiwa katika shambulio hilo, amesema hayo Meena Rai , ambaye amekuwa akifanya ununuzi kwa ajili ya maandalizi ya haurusi hiyo na marehemu. Harusi ilikuwa inatarajiwa kufanyika mwezi Februari mwaka ujao.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Bruce Amani