Mwili wa Kim Jong-Nam warejeshwa nyumbani
31 Machi 2017Mwili huo umewasili Pyongyang pamoja na raia watatu wa Korea Kaskazini ambao wanatakiwa kuhojiwa juu ya mauaji ya kaka wa baba mmoja wa kiongozi wa taifa hilo Kim Jon -Un , baada ya Malaysia kukubaliana na mpango wa kubadilishana raia.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya China kupitia msemaji wake Lu Kang imethibitisha kwamba mwili wa Kim Jong tayari umewasili Korea Kaskazini katika kisa ambacho maafisa wa Marekani na Korea Kusini wanasema ni mauaji yaliyoratibiwa na taifa hilo lenyewe.
Hata hivyo msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje ya China hakutoa maelezo ya kina juu ya mpango huo wa kubadilishana ambao umeshuhudia Wakorea Kaskazini wakirejea nyumbani kupitia Beijing.
Mamlaka za Malaysia ziliuruhusu mwili wa Kim hapo Alhamis katika makubaliano yaliyopelekea kuachiwa kwa Wamalaysia tisa waliokuwa wakishikiliwa mjini Pyongyang kufuatia mvutano wa kidiplomasia uliokuwa unaanza kuchomoza.
Kim ambaye amekuwa akiishi uhamishoni kwa miaka kadhaa aliuawa mnamo Februari 13 katika uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur kwa kutumia sumu ya VX, kemikali iliyopo katika orodha ya Umoja wa Mataifa kama silaha ya maangamizi.
Polisi wa Malaysia wamewataja raia wanane wa Korea Kaskazini wanaotakiwa kuhojiwa katika kesi hii, wakiwemo watatu ambao waliruhusiwa kuondoka nchini humo Alhamis jioni.
Waendesha mashitaka wa Malaysia pia wamewafungulia mashitaka wanawake wawili mmoja raia wa Indonesia na mwingine Mvietnam kwa mauaji ya Kim, lakini maafisa wa Korea Kusini na Marekani wanasema mauaji hayo yamefanywa na Korea Kaskazini yenyewe.
Korea Kaskazini iliwazuwia kusafiri kwa raia wa Malaysia mapema mwezi huu, wakiwemo wanadiplomasia watatu na wanafamilia sita, wakiwemo watoto wanne.
Waziri mkuu wa Malaysia Najib Razak ambaye yupo ziarani India alitoa agizo la kurejeshwa kwa mwili huo lakini hakutaja jina la Kim.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Malaysia Anifah Aman amesema, "kama mnavyofahamu, mchakato wa uchunguzi wa mwili wa Kim Jong umekamilika na mwili umerejeshwa Jamhuri ya Kiemokrasia ya watu wa Korea Kaskazini kutokana na ombi la familia na vikwazo vya kusafiri kwa watu wa Korea Kaskazini wanaoonoka Malaysia navyo vimeondolewa."
Korea Kaskazini imeendelea kusisitiza kuwa mwili huo si wa Kim Jong Nam na kwamba ni wa Kim Cho, jina lililokuwa katika pasi ya kusafiria ya marehemu.
Makubaliano hayo ya kubadilishana raia yanahitimisha mvutano wa kidiplomasia uliodumu karibu wiki tatu, kati ya serikali ya Malyasia na Korea Kaskazini.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman