"Mwezi wa damu" wasisimua watazamaji
28 Julai 2018Tukio hilo liliingiliana na kukaribia sana kwa sayari ya Mars na dunia katika muda wa miaka 15, tukio ambalo ni la kusisimua angani.
Wakati sayari ya mwezi ambayo huongozana na sayari ya dunia wakati wote, ikipita taratibu angani, makundi ya watu walikusanyika duniani kote kuweza kupata kuona tukio hilo la kipekee ambalo ni nadra.
Mbali na ziwa Magadi, kilometa 100 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi, jamii ya vijana wa Kimaasai waliangalia kupatwa huko kwa kutumia teleskopu yenye nguvu iliyotolewa na familia inayoishi katika sehemu hiyo.
"Hadi leo nilidhani Mars, Jupiter na sayari nyingine ilikuwa ni fikira tu za wanasayansi," Purity Sailepo , mwenye umri wa miaka 16 aliliambia shirika la habari la AFP.
Lakini sasa nimeiona na naweza kuamini na nataka kuwa mtaalamu wa mambo ya anga ili kuwaeleza watu wengine." Tofauti na kupatwa kwa jua, watazamaji hawakuhitaji kukinga macho yao kwa kutumia miwani ili kuweza kutazama tukio hilo la nadra kutokea. Kwa karibu nusu ya dunia, mwezi ulikuwa kwa sehemu fulani ama kwa ukamilifu katika kivuli cha dunia kwa muda wa masaa sita na dakika 14.
Kipindi cha kupatwa kamili , kilichofahamika kama "kupatwa kamili", wakati mwezi uliopoonekana kuwa na giza zaidi , kilikuwa kwa muda wa saa moja na dakika 43.
Wakati huo huo, sayari ya mars ilionekana karibu na mwezi katika anga la usiku, ilionekana wazi kwa macho. Watalaamu wa anga ambao wanafanya shughuli hiyo kwa mapenzi yao tu katika kizio cha dunia cha kusini walikuwa katika nafasi nzuri ya kutazama tukio hilo,hususan kusini mwa Afrika , Australia, na Madagascar, licha ya kuwa tukio hilo pia lilionekana katika mataifa ya Ulaya , kusini mwa Asia na Amerika ya kusini.
Watu wengi watazama tukio hilo
Zaidi ya watu 2,000 ikiwa ni pamoja na watoto wengi wakiwa na vifaa vya kuona mbali walijikusanya katika mji mkuu wa Tunisia , Tunis.
"Ninamatumaini kwamba kupatwa huku kutatuletea furaha na amani," amesema Karima, mwenye umri wa miaka 46, bila ya kuondoa macho yake angani.
Hata hivyo , hali mbaya ya hewa ilizuia kuonekana kwa hali hiyo katika sehemu kadhaa za dunia. Mvua kubwa za majira ya monsuni na mawingu mazito vilizuwia kuonekana kwa mwezi katika eneo kubwa la India na majirani zake, maeneo ambayo yalipaswa kuwa na muonekano mzuri. Hata pia , watazamaji waliokuwa na shauku ambao walijikusanya katika vilima na fukwe za bahari katika kaunti ya Uingereza ya Dorset walibaki gizani kutokana na mawingu mazito.Wale waliojikusanya katika mji mkuu wa Brazil Rio de Janeiro walikuwa na bahati zaidi, wakiuona mwezi huo mwekundu katika anga iliyokuwa wazi wakiwa na simu zao na kamera.
"Nafikiri ilikuwa nzuri sana, na niliipenda sayari ya Mars zaidi, ambayo iliweza kuonekana karibu kabisa na mwezi," amesema Talita Olivera , mwenye umri wa miaka 34.
sayari ya Mars ilionekana kuwa kubwa kuliko kawaida na angavu zaidi, ikiwa kilometa milioni 57.7 kutoka sayari ya dunia katika mhimili wake kuzunguka dunia. Kupatwa kamili kwa mwezi kunatokea wakati dunia ikiwa katikati ya mwezi na jua, na kuzuwia mwanga wa moja kwa moja kutoka katika jua ambao kwa kawaida hufanya mwezi kung'ara kwa rangi nyeupe iliyochanganyika na njano.
Mwezi husafiri kwenda katika eneo maalum kila mwezi , lakini muelemeo wa mzunguko wake una maana kwa kawaida unapita juu au chini ya kivuli cha dunia, kwa hiyo miezi mingi tunapata mwezi mpevu bila ya kupatwa.
Wakati sayari hizo tatu zikiwa katika msitari mmoja , hata hivyo, hali ya hewa ya dunia inasambaza mwanga wa buluu kutoka katika jua wakati ikitoa mwanga mwekundu katika mwezi, na huupa mwezi rangi ya hudhurungi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Lilian Mtono