Mwenyekiti wa Posta ya Ujerumani atuhumiwa kuepa kodi
14 Februari 2008Mwenyekiti wa shirika la Posta nchini Ujerumani Klaus Zumwinkel amefikishwa kituo cha polisi kutokana na tuhuma za kukwepa kodi kwa miaka mingi.
Kwa mujibu wa habari,mwenyekiti huyo anatuhumiwa kuweka fedha kiasi cha Euro Milioni 10 nje ya nchi.
Maafisa wa polisi pamoja na mawakili wa serikali leo walisachi nyumba ya mkuu huyo wa shirika la Posta ya Ujerumani Klaus Zumwinkel anaetuhumiwa kutenda uhalifu wa kukwepa kulipa kodi kwa muda wa miaka mingi.
Polisi,mawakili wa serikali na maafisa wa idara ya kodi ,mapema asubuhi leo waliivamia nyumba yake katika mji wa Cologne na kuisachi.
Ofisi za bwana Zumwinkel kwenye makao makuu ya shirika la Posta mjini Bonn pia zilisachiwa.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari mtuhumiwa alifikishwa kwenye ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali.
Shirika la televisheni la Ujerumani limeripoti kuwa mtuhumiwa bwana Zumwinkel ambae amekuwa anaiongoza Posta ya Ujerumani tokea mwaka 1990, anatuhumiwa kuweka katika benki ya nchi za nje fedha kiasi cha Euro Milioni 10. Na katika hayo alisaidiwa na wakfu mmoja wa nchi za nje.
Habari zaidi zinadai kuwa bwana Zumwinkel aliunda wakfu nchi za nje ili kupata nafuu ya kodi. Na tokea miaka ya 80 amekuwa anaziepa idara za fedha na kupeleka fedha kwenye wakfu huo.
Mtuhumiwa pia alikuwa na mpango wa kupeleka fedha katika nchi za Asia.