1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenyekiti wa chama cha SPD amkosoa kansela Merkel

Josephat Charo26 Oktoba 2007

Kiongozi wa chama cha Social Democratic, SPD hapa Ujerumani bwana Kurt Beck, amekikosoa chama cha Christian Democtatic Union katika serikali ya mseto kwa kuwa na kigeugeu na kutokuwa na msimamo. Beck ameyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano wa chama cha SPD hii leo mjini Hamburg.

https://p.dw.com/p/C7gB
Kurt Beck
Kurt BeckPicha: AP

Kiongozi wa chama cha Social Democratic, SPD hapa Ujerumani bwana Kurt Beck, amekikosoa chama cha Christian Democtatic Union katika serikali ya mseto kwa kuwa na kigeugeu na kutokuwa na msimamo. Beck ameyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano wa chama cha SPD hii leo mjini Hamburg. Josephat Charo na maelezo zaidi.

Akijaribu kuongeza uungwaji mkono katika chama chake cha mrengo wa kati na kushoto na kuondoa wasiwasi kuhusu uongozi wake, bwana Kurt Beck amefungua mkutano wa siku tatu wa chama cha SPD kwa kumkosoa kansela wa Ujerumani Angela Merkel na chama chake, miaka miwili kabla uchaguzi mkuu mwingine ujao.

Hatua ya bwana Beck kumshambulia kansela Merkel haitarajiwi kuiathiri serikali ya muungano, ambayo imekuwa na kipindi cha miaka miwili bila misuko misuko kutokana na kuimarika kwa uchumi wa nchi na kupungua kwa idadi ya watu wasio na ajira. Hata hivyo lawama hizo zinaashiria kuanza kwa uhusiano baridi huku uchaguzi unaoonekana utakuwa na mashindano makali ya kampeni ukikaribia mnamo mwaka 2009.

´Tuwakumbushe wapigaji kura kwamba wanasiasa wa chama cha CDU waliahidi kuleta mabadilkko makubwa katika masoko na hivyo kutushinda katika uchaguzi wa mwaka 2005,´ amesema bwana Beck, akigusia kampeni ya chama cha Angela Merkel cha CDU dhidhi ya chama cha SPD na pendekezo lake la serikali ya mseto na chama kidogo cha Free Democratic, FDP.

Bwana Kurt Beck amesema katika msingi wake, chama cha kihafidhina bado ni chama cha waliberali mambo leo na wakaidi wa soko huru. Sasa wanajidai wanaunga mkono sera za kijamii lakini ukweli uliopo ni kwamba bado wanafuatilia malengo ya uliberali mambo leo.

Bwana Kurt Beck ambaye huenda akapingana na kansela Angela Merkel katika uchaguzi wa mwaka wa 2009 amekabiliwa na matatizo ndani ya chama chake cha SPD huku chama hicho kikiporomoka kwa asilimia 30 katika matokeo ya kura ya maoni kutoka asilimia 34.2 iliyoshinda mwaka wa 2005. Chama cha CDU kimejiongezea umaarufu kufikia asimilia 40 kutoka asilimia 34.2 mwaka wa 2005.

Bwana Beck, ambaye yuko nyuma ya kansela Merkel katika kura ya maoni kuhusu umaarufu wa kibinafsi, ameapa kwamba chama cha SPD hakitamruhusu kansela Merkel avune faida za serikali ya mseto huku chama cha SPD kikipata lawama kwa makosa yaliyotokea na kushindwa kwa serikali katika utekelezaji wake wa kazi.

´Litakuwa jukumu letu katika kipindi cha muongo mmoja kuhakikisha kwamba ufanisi wa kiuchumi, jukumu la kuyalinda mazingira na usawa wa kijamii ni maswala muhimu nchini Ujerumani na yanabakia kuwa hivyo.´

Katika hotuba kwa wajumbe 525 iliyodumu muda wa saa mbili, bwana Beck pia aliwashambulia mawaziri wa chama cha CDU Wolfgang Schäuble, Franz Josef Jung na Michael Glos kwa kusababisha wasiwasi wa kufanywa mashambulio ya kigaidi hapa Ujerumani miongoni mwa mambo mengine.

Kurt Beck, akiwa waziri mkuu wa jimbo la Rheinland- Palatinate, ambaye hana kiti katika baraza la mawaziri, anagombea awamu nyengine ya miaka miwili kama mwenyekiti wa chama cha SPD. Viongozi watatu wa chama hicho wanagombea bila kupingwa kuchukua nafasi tatu za manaibu wa mwenyekiti wa chama, wakiwemo waziri wa fedha, Peer Steinbrueck na waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, ambaye huenda pia akawania ukansela mwaka wa 2009.

Kansela wa zamani wa Ujerumani, Gerhard Schroeder, amekishawishi chama cha SPD katika hotuba yake fupi kimuunge mkono bwana Beck licha ya mpango wake kurefusha faida za wafanyakazi wazee kwa miezi 24, jambo ambalo huenda likakwamisha mpango muhimu wa Schroeder wa mabadiliko ya kiuchumi yanayopendelea biashara.