Mwendesha mashtaka mkuu wa Ujerumani afutwa kazi
5 Agosti 2015Watetea haki za binadamu nchini Ujerumani wameushangiria uamuzi wa Waziri Maas wa kumwachisha kazi mwendesha mashtaka mkuu wa serikali, Harald Range.
Waziri Maas aliichukua hatua hiyo hapo jana kutokana na kuibuka mzozo juu ya tuhuma za uhaini. Mwendesha mashtaka huyo alianzisha uchunguzi dhidi ya blogi inayoitwa "Netzpolitik" iliyochapisha mipango ya idara ya usalama wa ndani ya Ujerumani juu ya kuupanua wigo wa upelelezi wa intaneti.
Waandishi wawili wa blogi hiyo walituhumiwa kutenda makosa ya uhaini kwa kuzichapisha habari hizo na mwendesha mashatka mkuu wa serikali alianzisha uchunguzi dhidi yao. Kutokana na uchunguzi huo waziri huyo wa sheria hapo jana alimchukulia hatua mwendesha mashtaka huyo na kutangaza kumteua mwendesha mashtaka wa Munich, Peter Frank, kuchukua nafasi ya Bwana Range.
Waziri Maas alisema alimpa taarifa Bwana Range ya kutokuwa na imani naye, na kwa hivyo kwa kuungwa mkono na Kansela Angela Merkel na kwamba angemuomba Rais Joachim Gauck amwezeshe mwendesha mashtaka mkuu huyo kustaafu.
Hata hivyo Bwana Range mwenye umri wa miaka 67 na aliyekuwa ameshapanga kustaafu mwaka ujao, alisema hapo awali kwamba kujiingiza katika mchakato wa uchunguzi ati kwa sababu unaweza kuathiri siasa za nchi ni kuhujumu uhuru wa mahakama.
Mihimili yavutana
Baadhi ya wanasiasa wamesema waziri wa sheria amevuuka mipaka kwa kumwachisha kazi mwendesha mashtaka mkuu na kudai kuwa waziri huyo amelipiza kisasi. Baada ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali kuuanzisha uchunguzi dhidi ya blogu ya "Netpolitcs", mvutano ulianza baina ya mihimili ya mahakama na dola.
Hapo jana, Waziri Maas alisema wizara yake ilimpa agizo mwendesha mashtaka mkuu la kutoitoa ripoti ya wataalamu iliyobainisha kwamba hati zilizochapishwa na waandishi hao wa habari zilikuwa siri za nchi. Kigezo hicho kilitosheleza kuanzisha uchunguzi juu ya tuhuma za uhaini.
Waziri Maas amesema hakuweza tena kuwa na imani na mwendesha mashtaka mkuu wa serikali baada ya mwanasheria huyo kuilaumu serikali kwa alichokiita kujiingiza katika uhuru wa mahakama.
Wakati huo huo, Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE) lilitoa mwito wa kuusimamisha uchunguzi uliokuwa unafanywa. Shirika hilo lilimwandikia barua Waziri wa Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, likitaka uhuru wa vyombo vya habari uheshimiwe.
Mkuu wa kitengo cha vyombo vya habari kwenye shirika hilo, Dunja Mijatovic, amesema kitisho cha kushtakiwa kwa uhaini ni jambo la kuwashtua waandishi wa habari wanaoandika juu ya habari za uchunguzi.
Mwandishi: Abdu Mtullya/AFP/DPA
Mhariri: Josephat Charo.