ICC yataka kukamatwa kwa mtawala wa kijeshi wa Myanmar
27 Novemba 2024Jenerali Min Aung Hlaing, aliyechukua madaraka kutoka kwa kiongozi aliyechaguliwa na wapiga kura Aung San Suu Kyi katika mapinduzi ya 2021, anatuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwa kufukuzwa na kuteswa Warohingya. Karibu watu milioni moja walilazimika kukimbilia nchi jirani Bangladesh kutoroka kile kilichoitwa kampeni ya maangamizi ya kikabila iliyohusisha ubakaji, mauaji na kuchomwa moto makazi. Kutoka kambi ya wakimbizi nchini Bangladesh, mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Karim Khan amesema katika taarifa kwamba anakusudia kuomba vibali zaidi vya kukamatwa kwa viongozi wa Myanmar hivi karibuni. Amesema katika kufanya hivyo, mahakama hiyo itakuwa inaonyesha kwa pamoja na washirika wake, kuwa WaRohingya hawajasahaulika. Kwamba wao, kama tu walivyo watu wengine kote duniani, wana haki ya kulindwa na sheria.