1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Mwanzo mpya wa amani Colombia

27 Septemba 2016

Makubaliano ya kiihistoria yamefikiwa kati ya serikali ya Columbia na waasi wa FARC. Colombia imefungua ukurasa mpya, ishara ya kumalizika mapigano ya zaidi ya miaka 50 yaliyosababisha vifo vingi.

https://p.dw.com/p/2Qd9R
Kolumbien Unterzeichnung des Friedensvertrags
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Vergara

Umoja wa Ulaya umeliondoa kundi la waasi la FARC la Columbia kutoka kwenye orodha ya makundi ya kigaidi baada ya kundi hilo kutia saini makubaliano ya amani kati yake na serikali ya Columbia. Makubaliano hayo ya kiihistoria yamefanyilka katika mji wa Catagena. Columbia imefaulu kufungua ukurasa mpya baada ya mapigano ya takriban miaka 50 na kuweza kuuonyesha ulimwengu kuwa amani inaweza kupatikana.  

Hatua hiyo inatazamiwa kuleta mafanikio. Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya ni kwamba hata baada ya kutolewa kwa kundi hilo la FARC kwenye orodha ya makundi ya kigaidi bado litaendelea kuwa chini ya makundi yanayo fuatiliwa kwa karibu  ikiwa ni pamoja na mienendo ya wanachama wake, isipokuwa vikwazo vilivyokuwa vimewekewa kundi hilo kama kutaifishwa kwa mali zao au vikwazo vya kifedha vitalegezwa. Hiyo ina maana kuwa watu au mashirika ya Umoja wa Ulaya sasa yanaweza kutoa misaada ya kifedha kwa kundi hilo linalo egemea mrengo wa shoto la FARC.

Vikwazo hivyo vitaondolewa kwa kipindi cha miezi sita kabla ya hatua hiyo kuangaliwa upya.  Kwa upande wake kundi la FARC limechukua hatua kadhaa nzuri jambo ambalo Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imepongeza lakini wakati huo ho kundi hilo limetakiwa kuendeleza mwendo huo mzuri hata baada ya kutia saini makubaliano ya amani ndipo liweze kutolewa kabisa kutoka kwenye orodha ya makundi ya kigaidi.

 Kwa Wakolumbia usiku wa giza la kutisha umemalizika

Waasi wa kundi la FARC
Waasi wa kundi la FARCPicha: picture-alliance/dpa/M. Duenas Castaneda

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mchakato wa miaka minne uliolenga kumaliza mapigano makubwa yaliyokuwepo katika Amerika ya kati na yanatazamiwa kuidhinishwa katika kura ya maoni wiki ijayo.Rais Juan Santos baada ya kutia saini Makubaliano hayo amewataka Wakolombia kuwa na matumaini mema na kusahau yaliyopita.

Serikali ya Columbia inakisia kwamba kiasi cha watu 260,000 wameuwawa katika mapigano hayo ya muda mrefu, hadi sasa takriban watu elfu 45 hawajulikani walipo huku zaidi ya watu milioni 6.9 wakiwa wameyahama kabisa makaazi yao.

Umoja wa Ulaya umesema kuwa utaendelea kuunga mkono juhudi za kuyafanikisha makubaliano hayo kwa mujibu wa mkuu wa maswala ya mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya  Federica Mogherini, ameeleza kuwa Umoja wa Ulaya uko tayari kutoa kiwango cha Euro milioni 600 kwa ajili ya kuunga mkono makubaliano hayo ya amani. Bibi Mogherini ameongeza kusema  kuondolewa kwa vikwazo kutaziwezesha nchi zote za Umoja wa Ulaya kushiriki katika mchakato huo wa amani ya Columbia.

Mjumbe wa Columbia katika Umoja wa Ulaya Ana Paula Zacarias amesema ana matumaini kwamba  kundi la waasi wa FARC litaondolewa kabisa kutoka kwenye orodha ya makundi ya kigaidi baada ya miezi sita hatua itakayo wezesha kufanyika kwa mazungumzo baina ya Umoja wa Ulaya na wapiganaji wa kundi hilo la waasi.

Mapigano hayo nchini Columbia yalianzishwa na kundi la FARC mwaka 1964 baada ya vurugu za wakulima ambazo zilizimwa na jeshi la nchi hiyo, kwa miongo kadhaa mapambano yamekuwa baina ya kundi hilo linalo egemea mrengo wa shoto na wanajeshi wa serikali inayoegemea upande wa kulia pamoja na  makundi ya walanguzi wa dawa za kulevya. Chini ya makubaliano hayo ya amani kundi la FARC litaweza kuunda chama cha kisiasa.

Mwandishi: Zainab Aziz

Mhariri: Yusuf Saumu