1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwandishi wa Somalia asomesha Berlin

10 Julai 2007

Mashambulio, mauaji na wakimbizi ni mambo yanayotendeka kila siku nchini Somalia. Profesa Nuruddin Farah, mwandishi wa habari wa gazeti la “New York Times”, anayeshughulika pia na uandishi vitabu ameandika mengi kuhusu hali nchini Somalia.

https://p.dw.com/p/CHkF
Mjini Mogadishu
Mjini MogadishuPicha: picture-alliance/ dpa

Mwandishi Nuruddin Farah ameshapendekezwa mara kadhaa kupokezwa tuzo ya Nobel. Na katika kupindi hiki cha kianganzi anafundisha katika chuo kikuu cha Berlin ambapo mwandishi wetu Werner Bloch alikutana naye na kuzungumza naye juu ya hali ya Somalia.

Katika maisha yaka, Nuruddin Farah ameshawahi kufikwa na kila hatari iliyoko Somalia: kwa mfana kuporwa, kutekwa nyara, kufukuzwa na kuhukumiwa kunyongwa. Hata hivyo lakini Profesa huyu na mwandishi mwenye umri wa miaka 54 anapenda kuutembelea mji wa Mogadishu: “Naipenda Mogadishu, ijapokuwa mke wangu na marafiki zangu wanasema nimevurugika kichwa kwa kurudi katika eneo la vita bila ya kulazimishwa. Mogadishu lakini ni kama sehemu ya mwili wangu, ni tumaini langu. Na wala sina hofu. Kwangu mimi, uwezekano wa kupata ajali ya gari hapa Berlin ni sawa na uwezekano wa kuuawa mjini Mogadishu.”

Taarifa anazoziandika kwa ajili ya gazeti la Marekani la “New York Times” ni sawa na habari moja kwa moja kutoka jahanamu. Katika kitabu chake kimoja kilichopata umaarufu Profesa Farah anaeleza juu ya maisha ya chini katika nchi ambayo serikali imevunjika, hakuna mfumo wala utawala wa katikati. Nuruddin Farah anazifahamu pande zote za vita vya Somalia, ikiwa ni viongozi wa koo, wa kidini au wa makundi ya kijeshi. Profesa huyu lakini anakumbusha kuwa Somalia imeharibika kutokana na maslahi ya nchi za Kigeni akitaja Ethiopia na Marekani, Misri, Kenya pamoja na Iran. Yeye mwenyewe amejaribu kuwa mpatanishi kati ya makundi ya Waislamu na serikali ya mpito, lakini mazungumzo hayo yalivunjika baada ya jeshi la Ethiopia kuivamia Somalia.

Alipoulizwa kuhusu juhudi za nchi za Magharibi za kuisaidia Somalia au bara la Afrika kwa jumla, Profesa Farah anabeza na kusema haoni chochote kilichofanywa na nchi za G8, nchi tajiri zaidi duniani. Ahadi hazikutimizwa. Pia jeshi la Kijerumani halijapiga hatua mathubuti katika doria zake kwenye bahari ya Somalia. “Ombi langu ni kwamba Wajerumani wasaidie kuwafukuza maharamia. Jambo la kushangaza ni kuwa siyo wanamaji wa Ujerumani au wa Marekani walioweza kuwazuia maharamia ambao ni wengi. Ujerumani haikufanya chochote kuisaidia Afrika wakati wa uwenyekiti wake wa Umoja wa Ulaya.”

Tarehe 18 Julai, siku ya Jumatano wiki ijayo, kutafanyika mkutano mkubwa wa kitaifa wa maridhiano mjini Mogadishu. Nuraddin Farah anatoa mwito pande zote husika zialikwe, ikiwa ni pamoja na wafuasi wa mahakama za Kiislamu. Hadi sana hakuna ushahidi kwamba yapo makundi ya kigaidi ya kimataifa nchini Somalia. Lakini ikiwa wanamgambo wa Kiislamu hawataalikwa kwenye mkutano huu, kama inavyosemekana, basi huenda wakajitafutia ungwaji mkono kutoka kwa kundi la Al Qaida.

Mbinu binafsi anayoitumia Profesa Nuruddin Farah ili uisaidia Somalia ni kupitia uandishi wake. Anataka kuiokoa Somalia kwa msaada wa fasihi. Katika vitabu vyake ambavyo vinaeleza juu ya maisha ya jamii au koo fulani wakati wa hali ngumu ya kisiasa, anafufua sura ya Somalia ambayo haiko tena.
Profesa Farah anasema: “Nchini Somalia kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda wa miaka 16. Kila mara jina la nchi hiyo linapotajwa, watu wanasema: achana na Somalia, Somalia imekufa. Wasomali wengi wametoroka kutoka nchini mwao. Lakini badala ya kuandika juu ya nchi nyingine, kama Afrika Kusini ambako naishi kwa sasa, mimi napenda kuandika juu ya Somalia.”

Mwandishi Nuraddin Farah anasema matumaini yake ni kuwa, Somalia itanawiri tena katika vitabu vyake na pia katika mioyo ya wale wanaosoma vitabu hivyo.