Mwandishi apigwa risasi Somalia
30 Mei 2013Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, habari za tukio hilo zimetolewa na maafisa wa serikakali na waandishi wengine wa habari nchini humo. Mwandishi mmoja wa habari, mwakilishi wa kituo cha televisheni kinachoitwa Royal TV, chenye ofisi zake kuu mjini London, huko Uingereza alisema washambuliaji wasiojulikana walimshambulia Abdikadir Abdirasak Sofe, ambae pia anajulikana kwa jina la utani "Jijile".
Mkasa huo ulitokea wakati mwandishi huyo akirejea nyumbani kutoka kazini jana jioni. Shuhuda mmoja Ali Mohamed alisema watu wawili mmoja miongoni mwao akiwa ameshika bunduki aina ya AK-47, alimfyatulia risasi majeruhi.
Imeripotiwa mwandishi, Abdikadir Abdirasak Sofe ambae amejeruhiwa mara kadhaa kwa risasi katika maeneo ya juu ya mwili wake, alikimbizwa hospitali. Hata hivyo Mohamed Saleban ambae ni afisa wa jeshi mjini Kismayo amesema baadae watu ambao wanatuhumiwa kuhusika na jaribio hilo la mauwaji walitiwa mbaroni ingawa haikuweza kufahamika mara moja ni nini hasa ilikuwa nia yao.
Somalia ni moja kati ya maeneo hatari zaidi kwa waandishi wa habari ambapo kiasi ya waandishi 18 waliuwawa mwaka uliopita. Mohamed Ibrahim, kutoka umoja wa waandishi wa habari nchini humo alisema wanaalani vikali vitendo vya kuwafyatulia risasi waandishi habari.
Shambulio dhidi ya Sofe linafuatia mauwaji mengine ya waandishi habari wanne yaliyotokea mwaka huu. Somalia imevurugwa na mgogoro wa tangu mwala 1991, lakini serikali mpya iliyokuwa ikiungwa mkono na iliingia madarakani mwaka uliopita.
Hata hivyo, shambulio la mwandishi Sofe limefanyika katika eneo la kusini la bandari ya Kismayo, ambalo lipo katika mamlaka ya mtu aliyejitangaza kuwa rais wa kanda hiyo ambae ni mshirika wa majeshi ya Kenya yaliyomo katika operesheni ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Afrika katika eneo hilo.
Mwaka uliyopota wanamgambo wa Al-Shebab, ambao wana mfungano la mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda walifurushwa na majeshi ya Kenya na washirika wake wa Somalia katika mji wa Kismayo, ingawa bado kumekuwa na matukio ya mashambulizi ya kupangilia katika mji huo.
Sambamba na hayo bado kuna mapambano ya wapiganaji wa makundi ya kikabilia katika eneo la kusini mwa Jubaland ambalo kila kundi linawania kupata fursa ya udhibiti wa kiutawala ya eneo hilo.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman