1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanasiasa Steinbach ajitoa chama cha CDU

Sekione Kitojo
16 Januari 2017

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo (16.01.2017) wamejishughulisha na kujiuzulu mwanasiasa Erika Steinbach wa chama cha CDU, mkutano wa amani ya mashariki ya kati mjini Paris na habari bandia katika Facebook.

https://p.dw.com/p/2Vqw3
Deutschland Erika Steinbach tritt aus der CDU aus
Erika Steinbach aliyejiuzulu kutoka chama cha CDUPicha: picture alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Kuhusu mada ya kujitoa katika chama cha Christian Democratic Union, CDU  kwa mwanasiasa Erika Steinbach akipinga sera za  wakimbizi  za kansela  Merkel  gazeti  la  Stuttgarter Zeitung  liliandika:

Si lazima mtu awe mtume ili kuweza kusema kwamba kujitoa kwa Steinbach kutoka chama cha Christian Democratic Union, CDU, ni  sawa na kujitafutia umaarufu miongoni mwa wafuasia  wa kihafidhina wa siasa kali za mrengo wa kulia na sio hatua  ya  mwisho ya kukipatia silaha chama mbadala wa Ujerumani, AfD, ambacho tayari kilijaribu  kumvutia Steinbach kuwa mwanachama  wake baada ya kuvunjwa moyo na sera za kihadhina. Jina la Steinbach litaendelea kusikika mara kwa mara katika mpambano wa kuwania uchaguzi wa Ujerumani, lakini mhariri anasisitiza kwamba sio katika chama cha CDU.

Katika  mada  hiyo  hiyo gazeti  la Nordwest-Zeitung  kutoka Oldenburg mhariri  anaandika kwamba baada ya Steinbach kujitoa chama cha CDU hakuna shaka  tena kwamba wahafidhina nchini Ujerumani hawana tena makaazi. Mhariri alieendelea kuandika kwamba mtu  anatambua  hilo  kutokana  na  msingi  kwamba  tangu  wakati wa  mjadala  wa  kuelekea  mrengo  wa  kushoto  mwaka  2010, Steinbach hakuweza  kuficha  tena  msimamo  wake.  Matakwa  yake ni kuelemea  mrengo  wa  kulia  zaidi  na  ndio msimamo  wake kuhusu  demokrasia. Kansela pamoja  na chama chake lakini katika miaka iliyopita wamevunja sheria hiyo  muhimu. Baada ya hatua  ya kuiokoa sarafu ya euro, kuliingia mzozo wa wakimbizi. Ndio sababu wakati mhafidhina kama  Steinbach amezungumzia masuala  hayo  wakati  akitoa maelezo  juu  ya  kujitoa  kutoka katika chama  hicho.

Amani ya Mashariki ya Kati

Mada  nyingine  katika  magazeti ni  kuhusu  mkutano  wa amani  ya  mashariki  ya  kati  uliofanyika mjini Paris nchini  Ufaransa. 

Paris Nahost Konferenz
Mkutano wa amani ya mashariki ya kati mjini ParisPicha: Getty Images/AFP/B. Guay

Mhariri aliandika - Ufaransa  iliyaalika  mataifa  70  ambayo  yalituma  mawaziri  wake wa  mambo  ya  kigeni  ama  wawakilishi  wengine  katika  mkutano na  matarajio  yake  ni  kuimarisha  amani  katika  mashariki  ya  kati. Lakini  kulikuwa  na  hali  ya  kukatisha  tamaa  katika  mkutano  huo. Msimamo  wa  suluhisho  la mataifa  mawili  unaporomoka, kulikuwa na  hamasa  lakini, kwa  hali  halisi, ujenzi wa makaazi  ya walowezi  wa  Kiyahudi katika eneo la ukingo  wa  magharibi, hatua ya  Israel  kuyumbisha  mazungumzo, na  tatizo  ambalo halijapatiwa  ufumbuzi  la  Ukanda  wa  Gaza,  yote  hayo hayajabadilika. Wasiwasi  umetanda  kimataifa  kuhusu  suala  hili, hususan  kutokana  na  ujumbe  wa  rais  mteule  wa  Marekani Donald Trump kabla  ya  kuingia  katika  ikulu  ya  Marekani,  White  House.

Taarifa za uwongo

Kuhusiana na  suala  la  taarifa  za uwongo katika  mtandano wa kijamii wa Facebook mhariri  wa gazeti la Frankfurter Rundschau aliandika: Kampuni  ya  Facebook kwa muda wa mwezi mzima haikuchukua hatua yoyote  kuhusu  athari, kuhusiana na suala la  taarifa bandia.  Sasa  Facebook imezungumza dhidi ya taarifa hizo bandia. Huo ni  uamuzi  ambao umechelewa  mno.  Ni  muda  mrefu sana umepita ambapo kumekuwa na taarifa hizi chafu za kihalifu. Mhariri  alisisitiza  kwamba muda umefika kwa facebook kutambua wajibu wake kabla ya uchaguzi mkuu nchini Ujerumani.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / Inlandspresse

Mhariri: Idd Ssessanga